THE WORLD BANK GROUP A World Free of Poverty
Home
[Back to TOC]

Maarifa ya Asili na Haki za Uvumbuzi

Biashara ya kimataifa katika rasilimali za kijenetiki, ambayo aghalabu hujulikana kama bio- biashara, siku hizi hufikia madau makubwa ya kiuchumu. Uuzaji wa madawa ya asili peke yake hufikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 32 (bilioni 1 = milioni 1000) kwa mwaka. Imekadiriwa kwa kuwauliza wenyeji watafutaji madini (bio – prospectors) wanaweza kuongeza uwiano wa mafanikio kutoka 1 katika sampuli 10,000 hadi kufikia 1 katika 2. Kwa uzoefu wa mtaalam mwingine, maarifa ya asili huongeza ufanisi wa kuchuja miti kwa ajili ya dawa kwa zaidi ya asilimia 400. Bila mchango wa maarifa ya asili, madawa mengi muhimu yanayotumika sana sana yasingekuwepo.

Kabla ya 1992, maarifa na rasilimali za asili vilichukuliwa kuwa ni urithi wa wanadamu. Hapakuwepo na sheria za kimataifa (na katika nchi nyingi, sheria za kitaifa) zilizodhibiti ufikio wa rasilimali za kijenetiki. Kutokana na hali hiyo kulikuwepo na ongezeko la matumizi ya maarifa na rasilimali za kibiolojia za wenyeji. Kwisha kwa haraka kwa rasilimali za kimazingira na haja ya kuwazawadia watumiaji na watoaji, kulipelekea uanzishwaji wa mapatano juu ya Bioanuwai (Convention on Biological Diversity – CBD), ambayo kwa mara ya kwanza yalitambua thamani ya maarifa na rasilimali za asili. Mapatano yaliweka utaratibu wa ufikio wa rasilimali za kijenetiki na wa mgawanyo wa haki na sawa wa faida.

Uvumbuzi ni njia ya kupata umilikaji wa rasilimali fulani mahususi. Kwa kawaida huhusu ulinzi wa kitu kilichovumbuliwa. Uvumbuzi huo huwa wa vitu vipya mbalimbali kama vile muziki, riwaya, madawa, programu za kompyuta na matokeo mengine ya matumizi ya maarifa ya asili.

Mapatano ya Bioanuwai yalianzisha dhana ya haki za uvumbuzi kama mkakati wa kuhifadhi bioanuwai kwa kuzipatia nchi haki juu ya rasilimali zake. Mpango huu ulijalizwa na Mkataba juu ya Haki za Uvumbuzi za Kibiashara (Agreement on Trade – Related Intellectual Property Rights – TRIPS). Kujumuishwa kwa Mkataba wa “TRIPS” katika mfumo wa WTO kulianzisha masomo mapya kwa nchi nyingi kuhusu hataza, hatimiliki, alama za kijiografia, majina ya kibiashara na ubunifu wa viwanda. Lengo kuu la Mkataba ni kuweka kiwango cha kimataifa cha ulinzi wa haki za uvumbuzi.

Haki za Uvumbuzi:mgogoro au nguvu zaidi

Je, ulinzi wa maarifa na rasilimali za asili kupitia haki za uvumbuzi huongeza ama huzuia upelekaji sawa wa faida za kiuchumi kwa wavumbuzi? Wahakiki wanadai kwamba haki za uvumbuzi ni tishio kwa bioanuwai kwa vile huzuia ufikio wa rasilimali na wa mazao yanayotokana na rasilimali hizo. Haki hizo huyafanya makampuni kuwekea hataza uvumbuzi unaotokana na maarifa na rasilimali za asili, bila kugawana kwa usawa faida za kibiashara na jumuiya zinazohusika na uvumbuzi. Watetezi wa Mkataba wa “TRIPS” hudai kwamba mkataba huo kuhamasisha uhumishaji wa teknlojia, ambao unaweza kuwa mkakati mmojawapo wa ugawanaji sawa wa faida. Yapo masuala mengine kadhaa ambayo huibuka katika mjadala huu. Haya yatazingatiwa na kurekebishwa kwa kuangalia mikakati ya kufanya kazi kwa kutumia haki za uvumbuzi zilizopo na, pale inapowezekana, kuzipanua zaidi kwa lengo la kuhifadhi maarifa ya asili na bioanuwai.

Matatizo ya utumiaji

Hali ya ubinafsi wa haki za uvumbuzi huleta matatizo kadhaa zinapotumika kwa jumuiya. Haki hizi hushindwa kuzingatia ukweli kwamba jumuiya huwa na mkabala jumlifu kwa mazingira yake. Jumuiya za namna hii huona vigumu sana kuzichukulia rasilimali wanazozitegemea kwa maisha yao kuwa rasilimali mahususi za kiuchumi na kijamii.

Mintarafu haki za uvumbuzi, jambo hili hupelekea kwenye tatizo jingine kubwa. Jinsi gani mtu afasili uvumbuzi na wafaidikaji wa uvumbuzi huo katika jumuiya, ikizingatiwa haja ya kuthibitisha upya na udhahiri wa hicho kilichovumbuliwa. Katika jumuiya nyingi za kimapokeo, watu hujifunza maarifa kwa muda mrefu na kuyasambaza kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kwa njia hiyo, haya maarifa daima hukua na kubadilika. Hivyo ni vigumu kubaini ni lini hasa maarifa fulani yaligunduliwa na lini yaliingia kwenye jumuiya.

Sehemu ya pili ya tatizo hili inahusisha ujumuiya wa maarifa ya asili. Ukuzi wa maarifa huchangiwa na wanajumuiya kama vile wazee ambao hekima na uzoefu huongeza thamani ya maarifa hayo. Kwa hali hii maarifa daima yamechukuliwa kuwa ni ya jumuiya na hivyo kushindwa kupata kigezo cha udhahiri wa hataza. Na endapo jumuiya nzima inahusika na ukuzi wa maarifa ya kimapokeo, mvumbuzi binafsi atatambulika vipi? Tatizo huwa kubwa zaidi pale ambapo maarifa ya asili yaleyale hutumiwa na jumuiya mbalimbali duniani kote. Kwa mfano, kama mitishamba fulani hutumiwa na Wamasai nchini Kenya, na pia Wahindi wa Amazoni, mvumbuzi halisi wa mitishamba hiyo atatambulika kwa kutumia njia ipi?

Tuongeze nguvu zaidi

Matatizo yaliyojadiliwa hapo juu yanaweza kupatiwa ufumbuzi kupitia mkataba wa “TRIPS” kwa kutumia namna mbalimbali za haki za uvumbuzi. Hizi hujumuisha alama za kijiografia ambazo hutumiwa zaidi kwa uvumbuzi unaofanywa na jumuiya. Njia nyingine ni kupanua dhana ya haki za uvumbuzi ili kujumuisha haki zenye msingi wa kijumuiya. Hii yaweza kujumuisha aina za kipekee za ulinzi zenye ubunifu zaidi kuliko matumizi ya hataza.

Baadhi ya watu wanapendekeza kurekebisha sheria za hataza ili kuhakikisha maombi yote ya hataza yanaonyesha  nchi chimbuko ya maunzi ya kibiolojia na maarifa ya asili yaliyotumika katika kufanya uvumbuzi. Jambo husianifu na hataza za maarifa ya asili ni haja ya kuzipatia hati rasmi. Tatizo la maarifa mengi ya asili ni kwamba hurithishwa toka kizazi kimoja hadi kingine kupitia mapokeo ya mdomo na siyo na rekodi za maandishi. Ili kuzuia maarifa ya kimapokeo ya jumuiya fulani yasichukuliwe kuwa yamevumbuliwa upya katika nchi nyingine ni muhimu maarifa hayo yakawekwa katika maandishi. Kwa kutumia njia hii jumuiya za kiasili zinaweza kupinga hataza zinazotolewa kwa watu wengine kwa maarifa ambayo ni yao kimapokeo. Kituo cha data za Maarifa ya Asili cha Benki ya Dunia na hatua kama hizo za WIPO za kusajili uvumbuzi wote wa kimapokeo vinalenga kuwezesha utekelezaji wa azima hii.

Zaidi ya hapo, uanzishaji wa rejista za maarifa ya kimapokeo za kitaifa, kikanda na kimataifa utawezesha ugawanaji mzuri wa faida miongoni mwa viwanda na jumuiya. Rejesta hizo zitasaidia juhudi zinazohusu haki za uvumbuzi kama vile kuimarisha hadhi ya maarifa ya kimapokeo kama sanaa awali, na hivyo kuwezesha kuwepo kwa “machapisho yanayolindika”.

Licha ya hataza, zipo njia nyingine za kuanzisha haki za uvumbuzi kwa maarifa na rasilimali za asili. Hizi zinajumuisha alama za kijiografia (majina ya mahali au maneno yanayohusiana na mahali yanayowezesha kutambua asili, aina na ubora wa kitu kilichovumbuliwa kwa mfano “chai ya Darjeelina”). Alama hizi ni nzuri kutunzia mapokeo ya pamoja huku zikiruhusu kutokea mabadiliko. Zinasisitiza mahusiano kati ya tamaduni za kibinadamu na mazingira yao na huweza kuhifadhi kadiri mapokeo ya kijumla yatakavyodumu. Haijali kama mvumbuzi ni mtu binafsi, familia ama shirika kubwa. Jumuiya za wenyeji hudai maarifa yao yasichukuliwe hivihivi tu kiholela. Hali kadhalika, alama ya kijiografia hufanya uvumbuzi usihamishwe kiholela.

Aina nyingine za ulinzi ni pamoja na hatimiliki na siri za kibiashara. Hatimiliki aghalabu hutumika kuzuia sanaajadiia ya kimapokeo isinakiliwe bila ruhusa maalum. WIPO imelinda sanaajadiia kutoka sehemu mbalimbali za dunia kama hatimiliki. Siri za kibiashara ni mbinu ya kulinda taarifa za siri zinazoweza kuwapatia wengine, kama vile mashirika ya kibiashara, unafuu wa ushindani. Siri hizi zinaweza kuwa njia thabiti ya kulinda maarifa ya asili. Jumuiya enyeji zingedhibiti ufikio wa maeneo na taarifa kwa watu wa nje kwa kutumia mikataba inayohakikisha kuwepo kwa siri na faida za kiuchumi. Mbinu za aina hii zimeshaanzishwa katika nchi kama vile Ecuador kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya Amerika (Inter – American Development Bank).

Jambo la pekee:ufikio na ugawaji sawa wa faida

Baadhi ya mabishano makubwa yanayohusu haki za uvumbuzi ni yale ya ulinzi wa spishi za mimea. Mkataba wa “TRIPS” unasema kwamba nchi wanachama zinaweza kutoingiza kwenye hataza “mimea na wanyama isipokuwa vidubini (vijiumbe) na hasa mifanyikotendani ya kibiolojia kwa ajili ya uzalishaji wa mimea na wanyama isipokuwa ile isiyo ya kibiolojia na ya kimikrobiolojia. Hata hivyo, nchi wanachama zitalinda mimea mbalimbali ama kwa kutumia hataza au mfumo thabiti wa kipekee au mbinu zozote mchanganiko”. – (Kifungu 27.36).

‘Mfumo wa kipekee’ ni mbinu za ulinzi ambazo hazitumii hataza. Mbinu inayojulikana sana ni ile inayohusisha “haki za wazalishaji wa miti”.  Katika kiwango cha kimataifa, nchi kadhaa zimejiunga katika Umoja wa Kimataifa wa Ulinzi wa Aina Mpya za Mimea (International Union for the Protection of New Varieties of Plants – UPOV) na baada ya majadiliano zikafikia makubaliano ya Ulinzi wa Aina Mpya za Mimea (Convention for the Protection of New Varieties of Plants). Makubaliano haya yameweka viwango vya chini kabisa vya ulinzi ambavyo vyapaswa kuzingatiwa na kila nchi. Pia huwawezesha wazalishaji miti kufaidika na “marupurupu ya wazalishaji” ambayo huwapa uhuru wa kutumia mimea inayolindwa katika programu zao za uzalishaji miti ili kuzalisha aina mpya za mimea.

Aina hii ya ulinzi inaelekea kupingwa na baadhi ya nchi zinazoendelea, lakini bila sababu za msingi. Kwa mfano, hofu kwamba wakulima hawataruhusiwa kuendelea na kilimo chao cha kimapokeo kutokana na njia hizi za ulinzi wa mimea, haina msingi wowote. Zao au jambo ambalo limekuwa likitumika wazi na umma sio jipya na hivyo haliwezi kupatiwa hataza. Ni aina mpya tu za mimea ndizo zitakazolindwa, na hata hivyo ni jukumu la mzalishaji miti kutafuta ulinzi huo. Ulinzi si jambo la lazima. Hivyo, wakulima wataweza kuhifadhi mbegu kutokana na mavuno yao kwa ajili ya kupanda kwenye ardhi yao (hii hujulikana kama “marupurupu ya wakulima”).

“Ulinzi wa Kipekee” unatoa fursa ya kwenda mbele zaidi ya haki za uvumbuzi na kuangalia mbinu nyingine za kurekebisha ufikio wa rasilimali na mgawanyo wa haki wa faida. Mbinu hizo zinaweza kujumuisha mikataba kati ya watumiaji na wamiliki wa rasilimali zenyewe, kama vile mikataba ya uhamishaji wa maunzi (Material Transfer Agreements). Nchini Cameroon, mathalani, Taasisi ya Taifa ya Kansa ya Marekani ilitiliana saini mkataba na serikali kufuatia ugunduzi wa spishi fulani za mimea zenye kemikali inayofaa kutengenezea dawa ya UKIMWI. Cameroon hutoa sampuli za miti hiyo na kulipwa fedha ambazo hutumika kwenye miradi ya maendeleo ya wanajumuiya ya kuhifadhi misitu.

Watu wengine wanadai kuwa mfumo wa “ulinzi wa kipekee” ambao unaruhusu kuwepo kwa ubunifu zaidi katika ulinzi wa mavumbuzi, unapaswa upanuliwe zaidi ili ujumuishe haki za kijumuiya na haki za rasilimali za kimapokeo. Mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile Mtandao wa Dunia ya Tatu (Third World Network) yanatetea haki mbadala zinazoakisi utamaduni na maadili ya jumuiya enyeji. Mashirika haya yanadai kwamba ili kuzingatia ipasavyo nguvu ya mabadiliko ya maarifa ya kimapokeo, dhana ya “ubunifu” yapaswa kufasiliwa kwa mapana zaidi ya dhana ya ubunifu wa viwandani. Ufasili huo waweza kuzingatiwa kwenye haki za kijumuiya.

Wataalamu wametoa mkabala jumulifu zaidi unaounganisha haki za uvumbuzi na sheria na mazoea ya kijadi. Wanadai kuwa maarifa ya asili hayawezi kutengwa na haki nyingine za asili kama vile haki za binadamu, haki za kumiliki ardhi na kuwa na serikali huru. Suluhisho mojawapo lingekuwa kuwa na mkabala unganishi kwa kuanzisha haki za rasilimali ya kimapokeo ambazo zingezingatia kwa dhati misingi ya haki za jumuiya. Haki hizi zinaweza kuwa mwongozo wa kuanzisha haki nyingine kama vile haki za uvumbuzi wenye nguvu zaidi.

Hitimisho

Haki za uvumbuzi zinaweza kuwa njia inayofaa ya kulinda mifumo ya maarifa ya asili na mimea ya aina mbalimbali. Hali hii huhimiza umuhimu wa kuyaweka maarifa ya asili katika maandishi; ambayo baadaye yanaweza kutumiwa kupinga dai la kutoa hataza kwa maarifa ambayo tayari yanajulikana katika jumuiya. Pili, inasisitiza umuhimu wa aina nyingine za haki za uvumbuzi licha ya hataza kama vile alama za kijiografia. Hizi zaweza kuhitajika zaidi na jumuiya za kimapokeo zinazohitajika kudhibiti ufikio wa rasilimali zake, kwani zinaweza kutumika kwa maarifa yanayoendelea kubadilika kutokana na mchango wa jumuiya enyeji. Hii inatupelekea kwenye uwezekano wa kupanua Mkataba wa “TRIPS” ili kuhakikisha kwamba hataza zinaonyesha chanzo cha rasilimali za kijenetiki na cha matumizi ya maarifa ya asili na zinazingatia “njia za kipekee” za ulinzi wa haki za uvumbuzi kama zile za kijumuiya ili kuwezesha upatikanaji wa mgawano sawa wa faida.

*Makala hii iliandikwa na Siddharta Prakash, Mshauri wa Kanda ya Afrika ya Benki ya Dunia. Imechapishwa tena, ikiwa imefupishwa, kwa ruhusa ya mchapishaji wa awali: “Towards a synergy between biodiversity and intellectual property rights”, na S. Prakash, Septemba 1999, Journal of World Intellectual Property (Jarida la Haki za Uvumbuzi), Vol. 2, No. 5

[Back to TOC]


Footer