THE WORLD BANK GROUP A World Free of Poverty
Home

[Back to TOC]

AFYA: MAARIFA YA ASILI, FAIDA LINGANIFU

na Katy Moran

Tangu Mapatano kuhusu Bioanuwai (Convention on Biological Diversity – CBD) yalipoafikiwa huko Rio (Juni 1992), tumejifunza mengi kutokana na maelezo juu ya mahusiano mapya yaliyochochewa na CBD. Nchi zenye utajiri wa bioanuwai, tamaduni za kiasili na maarifa yao ya matumizi ya rasilimali za kibiolojia kama madawa, na makampuni yanayojitahidi kugundua tiba mpya kwa kutumia mimea inayotoa madawa, na maarifa ya asili – vyote hivi sasa vina shauku na lengo moja. Thamani ya mimea kwa ajili ya madawa sasa inajulikana zaidi na “haki za uvumbuzi” za madawa hayo zimeshajadiliwa duniani kote. Kwa hakika, haki za uvumbuzi limekuwa ni jambo la kawaida kwa udhibiti wa miliki ya wenyeji ya maarifa ya kimapokeo kwa lengo la kuhakikisha kuwa faida za uvumbuzi zinarejeshwa kwa tamaduni na nchi zilizo vyanzo vya uvumbuzi husika (Mays, et al., 1997). Lakini, kadiri muda unavyopita, kiwango cha kutoweka kwa spishi na tamaduni kinaongezeka na afya ya binadamu imezidi kuzorota kutokana na magonjwa ambayo bado hadi sasa hayana tiba. Tunawezaje kutumia mafunzo ya CBD na tukaharakisha kutafuta mbinu za utekelezaji wake? Je, nchi zinaweza kutoa fursa za utafiti na uwekezaji kwa makampuni, ambayo, kwa upande wake, yatauza bidhaa zao kwa bei nafuu? Je, kuna uchunguzi kifani wowote uliofanywa unaoonyesha uwezekano huu, na kuna maswali gani ambayo bado yanahitaji majibu.

Mimea kama madawa

Mjadala wa haki za uvumbuzi unaonyesha umuhimu wa bioanuwai kwa afya ya binadamu. Tangu zama za kale hadi sasa, mimea imekuwa msingi wa famasia. Spishi kutoka nchi za tropiki zina utajiri mkubwa wa bioanuwai na biokemikali kutokana, kwa kiwango fulani, na hali ya hewa ya maeneo hayo. Katika maeneo yenye halijoto wastani, majira ya baridi kali huwaua wadudu waharibifu wa mimea, na mimea inayohimili halijoto wastani husitawi majira ya kuchipua kabla idadi ya wadudu waharibifu wa mimea haijaongezeka. Lakini kwa vile spishi za tropiki haziathiriwi sana na wadudu waharibifu wa mimea wa majira mbalimbali, nyingi zimejitengenezea kinga ya kikemikali dhidi ya wadudu wengi waharibifu wa mimea. Kemikali hizi za mimea ya tropiki zilizoongeza ustahimilivu wa mimea hiyo dhidi ya bakteria na vijidudu vingine viharibifu zinaweza pia kutoa kinga na zikatumiwa kutengenezea dawa kwa afya ya binadamu. Leo hii, robo ya madawa yetu yanatokana na mimea. Katika nchi zinazoendelea, asilimia themanini ya wananchi wake hutegemea mimea kwa matunzo ya afya yao ya msingi.

Nchi

Nyingi ya nchi zenye utajiri wa bioanuwai hupatikana kwenye tropiki za Kusini, ilihali nchi zenye utajiri wa teknolojia, zenye rasilimali kwa ajili ya maendeleo endelevu ya bioanuwai, hupatikana zaidi Kaskazini kwenye halijoto wastani. Kabla CBD haijafungamanisha mataifa na bioanuwai zao, bioanuwai hizo zilichukuliwa kuwa ni “urithi wa binadamu wote”. Kila mtu aliruhusiwa kutumia rasilimali za kibiotiki, na zilikuwepo taratibu chache mno za kisheria za kurejesha faida zilizotokana na uvumbuzi wa madawa katika nchi zilizo chimbuko la uvumbuzi huo. CBD sasa inajitahidi kuleta urari wa jinsi wahusika wote wa harakati hizi wanavyoweza kufaidika na matumizi endelevu ya bioanuwai na viambato vyake. Nchi za Kaskazini zinaweza kutumia bioanuwai ya nchi za Kusini kwa kushirikiana teknolojia na faida inayotokana na matumizi ya kibiashara ya bioanuwai. Ni jukumu la kila nchi mwanachama wa CBD, hadi sasa ziko nchi 169, kutunga sera ya taifa ya bioanuwai ikielekeza namna ya  utekelezaji wa suala hili nchini, ikiwa ni pamoja na kutunga sheria za utekelezaji huo. Baraza la Utafiti wa Kisayansi na Viwanda la India, linalopata ruzuku kutoka serikalini, kwa mfano, hivi karibuni limeanzisha programu ya kuzuia uigaji wa uvumbuzi wake ili kulinda mkusanyiko wa maarifa yake kuhusu madawa yatokanayo na mimea.

Makampuni

Tangu CBD ianzishwe, hakuna dawa kutoka nchi za tropiki iliyotengenezwa kwa maarifa ya kimapokeo inayouzwa kibiashara. Faida za kiuchumi bado hazijapatikana. Utengenezaji wa dawa kwa kawaida huhitaji utafiti ghali na wa muda mrefu ili kupata ithibati ya serikali kabla dawa husika haijaanza kuuzwa. Nchini Marekani, dawa mpya huchukua, kwa kawaida, miaka 10 hadi 15 kuwa tayari kwa matumizi, baada ya uwekezaji wa zaidi ya $ milioni 300 na kampuni na wawekezaji wanaokubali kuchukua dhima ya kuitengeneza, kuifanyia majaribio na kuiuza dawa hiyo mpya. Kwa kampuni mpya, miundombinu kama vile majengo, vifaa na mishahara ya wanasayansi watafiti lazima vigharamiwe kabla dawa yenyewe haijaanza kuzalisha mapato. Ili kupata fedha hizi nyingi zinazohitaji kugharamia utafiti na maendeleo ya madawa, makampuni hutegemea mtaji wa kijasiri, faida za hisa, ubia na mashirikiano ya namna hiyo – uwekezaji na watu wa nje katika mradi wa kampuni wenye hatari nyingi, lakini pia wenye faida kubwa. Wawekezaji waweza kuwa watu binafsi ama mashirika na uwekezaji wao una hakimiliki ya ruhusa ya kutengeneza, kuuza, na kutumia madawa yatakayovumbuliwa. Hakimiliki hutoa kinga ya uvumbuzi kwa kampuni, na hivyo kuwawezesha wawekezaji kurejesha fedha walizowekeza kwenye utafiti na maendeleo ya madawa, pale madawa hayo yanapouzwa kibiashara. Hayamkiniki kwamba kampuni yoyote ama mwekezaji yeyote atahatarisha mtaji wake kugundua au kuendeleza dawa fulani bila uwekezaji huo kulindwa kwa hakimiliki dhidi ya ushindani na makampuni mengine.

Tamaduni

Asilimia sabini na nne ya madawa makuu 121 yatokanayo na mimea yana matumizi yanayofanana kwa tamaduni nyingi za asili. Badala ya kuchagua na kuichunguza mimea kiholela, mkakati ulio bora zaidi ni kwa baadhi ya makampuni kutumia maarifa ya asili ili kuitambua miti bora zaidi kwa madawa mapya. Lakini mikakati michache sana inayojishughulisha na jinsi maarifa ya asili yanavyoweza kufikiwa na faida linganifu zinavyoweza kugawanywa kwa kuzingatia utamaduni unaohifadhi mifumo ya kijamii iliyoujenga. Tofauti kati ya uchumi wa soko, uliokitwa kwa umiliki wa watu binafsi, na uchumi wa kijumuiya, ambao kwa kawaida huwezesha kumiliki pamoja rasilimali za kibiolojia na kiutamaduni, humaanisha kwamba kikundi kizima cha kitamaduni lazima kifaidike. Ni vikundi vichache sana vya asili vimeshirikishwa katika mijadala ya kitaifa kuhusu masuala haya, au kuhusu ufafanuzi na utekelezaji wa CBD katika nchi zao.

UCHUNGUZI KIFANI

Nigeria

Kiutendaji, uchunguzi kifani wa jinsi gani nchi mbalimbali, makampuni na tamaduni zinaweza kushirikiana na kutekeleza malengo ya CBD ni ule wa Kampuni ya Madawa ya Shaman (Shaman Pharmaceuticals, Inc.) ya Nigeria. Kwa mujibu wa daktari Tom Carlson, Mkurugenzi Mwandamizi wa Utafiti wa Uwandani wa Etinobiotiba wa kampuni ya Shaman, “Katika nchi hii ya Afrika Magharibi, yenye utajiri wa bioanuwai na tamaduni, mifumo ya dawa ya asili inasitawi sambamba na fursa za dawa za Magharibi. Mnamo mwaka 1995, serikali ya Nigeria iliwaunganisha rasmi waganga wa kienyeji katika huduma ya afya ya taifa kama watoaji wa matunzo ya afya na leo hii theluthi mbili ya watoaji wa matunzo ya afya ni waganga wa kienyeji wa namna moja au nyingine” (Carlson et al., 1997).

Nchini Nigeria, Profesa Maurice Iwu ni mwanasayansi na Mkurugenzi wa Programu ya Maendeleo na Hifadhi ya Rasilimali za Kibiolojia (Bioresources Development and Conservation Programme – BDCP), ambalo ni shirika lisilo la kiserikali (NGO) la Nigeria. Iwu anafafanua, “BDCP ilianzishwa mwaka 1991 kama kitovu cha mashirikiano ya kitafiti yanayojenga stadi za kiufundi nchini Nigeria ili kwamba rasilimali za kibiolojia ziwe chombo imara cha maendeleo endelevu. Stadi zilizoboreshwa zinapelekea kwenye uchunguzi wa makini zaidi wa madawa ya magonjwa ya kitropiki yanayopatikana kwa wingi nchini Nigeria kama vile malaria, leishimaniasisi, na tripanosomiasisi” (Iwu, 1996).

Kampuni ya Madawa ya Shaman

Kampuni ya Madawa ya Shaman ilianzishwa mwaka 1990 na, kupitia BDCP, ikaanzisha ushirikiano wa kitafiti na asasi za kisayansi za Nigeria, jumuiya za vijijini, na waganga wa kienyeji na vyama vyao. Kampuni hii ndogo, ambayo makao yake makuu yako California, ilianza utafiti ukilenga katika uvumbuzi na uendelezaji wa madawa mapya yanayotokana na mimea yenye historia ya kutumiwa na wenyeji. Lisa Conte, Rais na mwasisi wa kampuni anaelezea juu ya suala hili, “Kama jina lake linavyoashiria, Shaman hutumia sayansi ya etnobotania, na pia kemia ya kutenga na ya mazao asilia, sayansi ya tiba ya maradhi na famakolojia ili kupata mbinu bora zaidi ya ugunduzi wa madawa. Wakati ikiundwa kama kampuni ya kuzalisha faida, Shaman ilianzisha pia Hifadhi ya Msitu wa Madawa (Healing Forest Conservancy), shirika lisilo la kutafuta faida lililoanzishwa mahususi kutafuta utaratibu wa kurejesha faida kwa nchi na tamaduni zinazoshirikiana na Shaman baada ya madawa kuuzwa kibiashara.” Ingawa kampuni hii changa bado haijauza madawa yake, matumizi ya etnobotania katika utafiti yamewezesha dawa zinazotafitiwa na kampuni kuanza kufanyiwa majaribio ya matumizi mapema sana (King, et al., 1996).

Faida za Moja kwa Moja na za Muda wa Wastani Zilizosambazwa Nchini Nigeria

Iwu na mwanasayansi mwingine wa Nigeria, Cosmos Obialor, walipendekeza majadiliano ya awali na waganga na viongozi wa kimapokeo kuzungumzia juu ya kushirikiana na kampuni ya Shaman muda mrefu kabla ya kuanzishwa kwa CBD huko Rio mwaka 1992. “Tulizitembelea jumuiya ambako tulikuwa tumefanya kazi kwa miaka kadhaa,” alisema Iwu, “ikiwa ni pamoja na vijiji alikozaliwa Obialor na nilikozaliwa mimi. Kimsingi, kila jumuiya, au kijiji hujitawala chenyewe kikiwa na chifu na serikali yake. Utaratibu wao wa kufikia maamuzi ya kijumuiya hujumuisha chifu wa kijiji, washauri wake, waganga wa kienyeji na wazee,” aliongeza Iwu. Baada ya majadiliano ya muda mrefu, vikundi hivi viliafiki kwamba kampuni ya Shaman ilikuwa na malengo kama yao na yaliyozingatia utamaduni kuhusiana na afya ya binadamu. Kutokana na majadiliano haya na yale ya awali, sera mwafaka za ushirikiano na kampuni zilifikiwa. Majadiliano yaliyopelekea kwenye makubaliano yalihusu maswala kama vile nia na malengo ya mradi; vipi na wapi mimea itachanganuliwa; fursa ya kibiashara ya mimea hiyo na namna ya kugawana faida.

“Tangu wakati huo, utafiti wa uwandani wa kietnobotania umeshafanyika mara nne,” alisema Steven King, Makamu wa Rais Mwandamizi wa Etnobotania na Hifadhi wa Kampuni ya Shaman. “Kwa uchaguzi wa washirika wa Kinigeria, faida zimechukua umbo la warsha na programu za mafunzo juu ya afya ya jamii, botania, hifadhi na etnobotania; msaada kwa hifadhi ya mimea ya dawa; vifaa kwa ajili ya shule za vijijini; ukusanyaji wa vifaa vya kibotania kwa ajili ya hebaria (mahali pa kuhifadhia mimea iliyokaushwa); vifaa vya maabara kwa ajili ya utafiti wa kisayansi wa mimea inayotibu magonjwa ya vimelea yaliyoenea sana Afrika Magharibi na kuwasaidia wanasayansi wa Kinigeria ili waweze kutumia mbinu mpya za uchanganuzi. Kutimiza sera ya kampuni, faida za moja kwa moja na za muda wa wastani, kama za hapo juu, zenye jumla ya thamani ya dola za Marekani 200,000 (elfu miambili) zimegawanywa kupitia katika programu mbalimbali kwa washika dau wanaoshiriki katika mpango huu”.

Iwu aliongeza, “Kampuni hupeleka ripoti za uchunguzi wa maabarani mara kwa mara kwa jumuiya zinazoshiriki kwenye mradi. Maandiko ya kawaida kuchapishwa kuhusu mimea ya madawa kutoka Nigeria yakionyesha utambuzi wa umma wa faida za maarifa ya kimapokeo ya Nigeria kwa jamii na afya ya binadamu”.

Faida za Muda Mrefu

Baada ya madawa kuuzwsa kibiashara, kampuni ya Shaman itatoa asilimia fulani ya faida zake kwa Nigeria na makampuni mengine yaliyoshiriki mradini kupitia kwenye Hifadhi ya Msitu wa Madawa kwa kipindi chote kampuni itakapokuwa na faida. Hifadhi itagawa faida hizi, kwa usawa, kwa nchi na tamaduni zote zilizo washirika na kampuni ya Shaman, bila kujali nchi ama utamaduni ulio chanzo cha mmea wa dawa au maarifa ya kimapokeo yanayouzwa kibiashara. Katika mradi kama huu ambapo mapato yake ya kifedha hayatabiriki, kusambaza faida na hatari za hasara miongoni mwa washirika wote wa Shaman kunaongeza fursa za fidia (Moran, 1997).

Kampuni ya Shaman na Hifadhi zinafuata kanuni ya CBD kwamba wahifadhi wenyeji wa bioanuwai wanapofaidika kutokana na matumizi endelevu ya mimea yao ya madawa na watu wengine wa nje, basi fursa za uhifadhi huongezeka. Ili kuzuia shinikizo la uchumi mwingine ambao unaweza kuwa na athari mbaya kwa bioanuwai, faida za kuilinda bioanuwai hiyo lazima zionekane mahali bioanuwai ilipo. Hata hivyo, kukosekana kwa modeli mwafaka kunafanya nadharia tete hii isithibitishwe. Ili kujaribu uwezekano wa kutumia mapatano ya dhamana kama chombo cha kugawana faida, Hifadhi imetoa $ 40,000 (dola elfu arobaini) kwa mfuko wa dhamana nchini Nigeria kwa ajili ya mradi wa majaribio.

Mfuko wa Maendeleo Unganifu ya Vijijini na Madawa ya Kienyeji (Fund for Integrated Rural Development and Traditional Medicine – FIRD – TM), mfuko huru wa dhamana, ulianzishwa na BDCP kama chombo cha fedha kwa ajili ya maendeleo endelevu ya vijijini na kwa ajili ya kusambaza faida miongoni mwa washika dau wa Nigeria. Bodi ya mfuko huu inajumuisha vikundi vyote vya washika dau, yaani viongozi wa vyama vya waganga wa kienyeji, maofisa waandamizi wa serikali, wawakilishi wa mabaraza ya vijiji ya makabila mbalimbali na wataalam wa kiufundi kutoka kwenye asasi za kisayansi. Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi wa Mfuko, Mtukufu Eze E. Njemanze wa 0werri, ni mtawala wa kimapokeo anayeheshimika sana. Nafasi kubwa inayochukuliwa na mifumo ya mshikamano wa kimapokeo, kama vile vyama vya kikabila na vyama vya kitaalam vya waganga, hutoa muundo wa kijamii unaohakikisha ushiriki wa jumuiya. Vikundi mbalimbali vya kitamaduni vya Nigeria vitapatiwa fedha kupitia vyama vya waganga wa kienyeji na vijiji kulingana na desturi zao. Vyama vya mijini, wakuu wa vijiji na vyama vya kitaalam vya waganga vimepewa uwezo wa kufanya maamuzi kuhusu miradi ya maeneo yao. Miradi itakayopatiwa fedha itafuata vigezo vya kusitawisha hifadhi ya bioanuwai na kuendeleza madawa, na kadhalika usitawi wa kijamii na kiuchumi wa tamaduni za vijijini. Kwa ngazi ya kijiji, stadi za kiufundi zilizopatikana kutokana na kugawana faida husaidia kusanifisha na kukuza madawa fita (phytomedicines), kusambaza na kushirikiana taarifa zinazowafaidisha waganga wa kienyeji na afya za jumuiya wanazozihudumia.

Uzinduzi wa FIRD-TM ulitangazwa jijini Abuja, Nigeria, kunako Septemba 30, 1997, wakati wa kongamano la kimataifa juu ya mimea ya madawa lililohudhuriwa na mawaziri watano wa Nigeria na wakuu kadhaa wa mashirika ya serikali ya Nigeria, ikiwa ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Mazingira la Shirikisho la Nigeria. Waziri wa Makao Makuu ya Shirikisho ya Abuja alisema, “… stadi za waganga wa kienyeji ambao pia ni wahifadhi wa utamaduni wetu wa madawa ya asili sasa zinapatiwa nafasi yake mwafaka katika jamii”.

Dhana ya mfuko wa dhamana inatoa fursa zaidi ya kushawishi na kusimamia vyanzo vya fedha kutoka NGO nyingine, mashirika au makampuni yenye wito wa kuchangia katika mfuko ulio imara. Wakati mchango wa Hifadhi ulipotangazwa, Chama cha Wazalishaji wa Madawa ya Asili na Kampuni ya Madawa ya 0range za Nigeria ziliahidi kuchangia fedha zaidi kujaliza mchango wa Hifadhi. Mwaka ujao, mradi utatathiminiwa na kutumiwa kuiongoza Hifadhi kuanzisha mfuko wa dhamana wa kiolezo utakaotumiwa na washirika wote wa kampuni ya Shaman, makampuni na mifuko mingine ya kutoa misaada.

MASUALA YALIYOBAKIA

Uchunguzi kifani wa kampuni ya Shaman nchini Nigeria unatoa mfano wa jinsi nchi, vikundi vya utamaduni na makampuni yanavyoweza kushirikiana kwa faida ya washika dau wote kuleta maendeleo endelevu ya bioanuwai kwa ajili ya afya ya binadamu. Ni njia mojawapo ya kutimiza malengo ya CBD na kila mshiriki anapaswa kuendelea kutafuta, kubainisha na kuagiza mbinu mpya zinazofaa zaidi kwa mazingira yake. Nchi, tamaduni na makampuni yanayoshirikishwa yametofautiana mno kiasi kwamba hatua zinazochukuliwa zitafaa tu iwapo zitazingatia miktadha mahususi ya kiutamaduni, kiuchumi na kimazingira. Masuala yafuatayo bado hayajapatiwa ufumbuzi.

·         Nigeria ilitoa mkakati wa ushirikiano kwa ajili ya kampuni ya Shaman, kwa kushirikisha asasi zenye uwezo kamilifu, hasa kwenye ngazi ya kijiji. Mifumo hii inayojitegemea, ikiwa na machifu wao na serikali zinazofanya kazi, ilichagua kutumia maarifa yao ya kimapokeo kuhusu ulimwengu wa nje kufikia malengo ambayo iliyaona muhimu kwake. Vikundi mbalimbali vya asili vina imani zinazotofautiana kuhusu shughuli za biashara na vina mitazamo inayotofautiana kuhusu dhana ya soko. Tofauti hizi hazipashwi kamwe kuwa kisingizio cha kuvitenga vikundi vya kiasili na matumizi endelevu ya bioanuwai, kwani huu ndio uamuzi wao pekee wa kufanya, na sio ufanywe na NGO zisizo za kiasili, kama inavyofanyika mara nyingi, NGO zinazodai kuwakilisha mawazo ya wenyeji katika kutoa uamuzi juu ya masuala haya.

·         Kifungu 8 (j) ni sehemu ya CBD inayozungumzia kuhifadhi na kuheshimu maarifa ya asili. Lakini kinatoa ulinzi hafifu sana wa vikundi vya utamaduni na kina- lazimisha CBD ifuate sheria za nchi. Kisheria, ni washiriki wa CBD, sio sera za makampuni, wenye mamlaka ya kuamua jinsi ya kutekeleza maendeleo endelevu ya bioanuwai katika maeneo yao. Hali ya kisiasa ya nchi vinamoishi vikundi vya kiasili ni muhimu kwa mafanikio ya maendeleo ya bioanuwai. Kwa vile vikundi vya kiasili ni washika dau wakubwa wa masuala ya CBD, ni lazima vishirikishwe kwenye mijadala ya mataifa yao kuhusu ufafanuzi na utekelezaji wa CBD. Ili kuhakikisha kudumishwa kwa mifumo yao ya kiutamaduni, ni lazima vishiriki na vipigania vyenyewe masilahi yao. Kama nchi zinataka kufaulu vema kuhifadhi spishi za dunia, mikakati yao lazima ilenge kuwashirikisha watunzaji wa bioanuwai, na sio ilazimishwe juu yao kutoka kwenye ngazi za juu.

·         Kufungamanishwa kwa wenyeji na maeneo ya kimapokeo kunaongoza matendo yao yanayohusiana na ikolojia. Utambuzi wa kisheria na serikali wa haki za maeneo unavipatia mamlaka vikundi vya wenyeji kuwakatalia ama kuwaruhusu watu wa nje kuingia katika maeneo hayo – hatua ya kwanza ya kuhifadhi bioanuwai kupitia usimamizi wa kimapokeo wa ardhi na rasilimali. Lakini suala hili muhimu lilipewa uzito mdogo sana kwenye warsha ya hivi karibuni ya CBD iliyofanyika Madrid na kuhudhuriwa na wawakilishi wa serikali na vikundi vya wenyeji. Watu wengi waliona kuwa hii ilikuwa ni fursa iliyopotezwa. Wengine waliiona warsha hiyo kama hatua ya kwanza ambako maagizo ya kimaendeleo kuhusu hifadhi ya bioanuwai kupitia haki za maeneo, kama vile Sheria Na. 8371 ya Philippines, yangeweza kutangazwa. Jambo lililobaki ni kuangalia endapo katika mikutano inayofuata suala la hifadhi ya bioanuwai kupitia haki za maeneo litabanwa tena na madondoo mengine ya ajenda (Burgiel, et al., 1997).

·         Taarifa sahihi ni jambo muhimu. Ni wajibu kwa washika dau wote wa CBD kuwa na uelewa sahihi wa dhana ya haki za uvumbuzi. Haki hizi si mbadala wa haki za ardhi na haki za binadamu na kukatishwa tamaa hujitokeza pindi watu wanapojaribu kuzitumia haki za uvumbuzi kwa malengo yasiyo yake. Jambo litakalofaulu ni kwa nchi, tamaduni na makampuni kuchangia pamoja uzoefu wao, kwani hakuna mfumo mmoja pekee unaoweza kufaa katika mazingira yote. Hifadhi na maendeleo endelevu ya bioanuwai yanahitaji mikabala tofautitofauti.

Makala hii imerekebishwa kidogo kutokana na makala inayoitwa “Moving On: Less Description, More Prescription for Human Health” iliyoandikwa na Katy Moran, katika Ecoforum, Journal of the Environment Liaison Center International, Vol. 21, No. 4, Januari 1998. Kwa taarifa zaidi juu ya somo hili, tafadhali wasiliana na Katy Moran, Mkurugenzi Mtendaji, Hifadhi ya Msitu wa Madawa,

3521 S Street, NW-Washington, DC 20007.

<Moran HFC@aol.com>

 

[Back to TOC]


Footer