THE WORLD BANK GROUP A World Free of Poverty
Home

[Back to TOC]

Kutunza Mazingira Katika Pwani ya Magharibi ya Senegal

Hifadhi ya Asili ya Ker Cupaam iko katika eneo la “Petite Cote” la Senegal, kilomita 45 kusini mwa Dakar kwenye pwani ya Atlantiki. Sehemu hii ya msitu wa asili wenye ukubwa wa takribani hekta 100 ilitengwa kwa amri ya serikali mwanzoni mwa miaka ya 1980 ili kulinda makazi ya majira ya baridi ya ndege aina ya “blue grackle” na “rock grackle” ambao walikuwa hatarini kutoweka, na kuhifadhi njia wanayotumia ndege wengi wanaohamia kwenye pwani ya Atlantiki ya Afrika Magharibi. Majabali yanayopakana na ufuko kwenye eneo hili la pwani yanafaa sana kama mahali pa kuzalia na malisho kwa aina nyingi za ndege.

Mimea na wanyama wa eneo hili wameharibiwa vibaya kwa miaka mingi kutokana na athari za ukame, uchungaji unaovuka kiwango na ukataji kuni. Hata hivyo, pwani karibu na Popenguine ni kivutio kikubwa cha watalii kutoka Dakar na pia ni kituo muhimu cha hija kwa Wakatoliki. Lakini shughuli hii haijawaletea faida kubwa wenyeji wa eneo hili, na wengi wao wameanza kulalamika juu ya uzorotaji wa rasilimali yao hii.

Kukabili changamoto

Ingawa katiba ya hifadhi ya asili mwanzoni mwa miaka 1980 ilisaidia kusimamisha uharibifu zaidi wa mazingira, mimea mingi katika eneo ilikuwa imeharibiwa mno kiasi kwamba juhudi kubwa zilihitajika kurejesha ustawi wa zamani na kuvutia shughuli za kitalii ambazo zingewaletea faida wenyeji wa eneo hili. Hilo ndilo hitimisho lililofikiwa na kikundi cha wanawake kutoka kijiji cha Popenguine, ambao mwaka 1988 walianzisha Umoja wa Wanawake wa Popenguine wa Kuhifadhi Mazingira (Regroupment des Femmes de Popenguine pour la Protection de la Nature – au “RFPPN”). Kikundi kilijumuisha awali wanawake 119 na mwanamume mmoja, ambaye alitokea kuhudhuria mkutano wa uanzilishi wa Umoja huo. Walimchagua mungu Mame Cumba Cupaam, “roho wa wavuvi wa pwani”, kuwa matroni (mlezi) wao.

Katika kipindi cha miaka minane iliyofuata, umoja wa “RFPPN”  ulitumia kwanza rasilimali zake na kisha za nyongeza kutoka kwa mashirika ya wafadhili yaliyounga mkono usimamizi wa aina hii wa maliasili ili kurejesha upya ustawi wa awali wa mimea ya hifadhi na eneo la karibu na hifadhi. Hatua zilizotekelezwa na Umoja huu ni pamoja na utengenezaji wa vizuizi vya moto kuzunguka hifadhi yote, upandaji upya wa mimea ya asili kwa eneo hili kwa kutumia miche ya kitalu kilichoanzishwa sawia na wanawake, na kuandaa warsha ambapo vijana wa kujitolea kutoka vijiji na miji jirani waliletwa kujifunza hifadhi ya maliasili na kufanya kazi kwa vitendo iliyohitajika.

Kwenda kwenye kiini cha jambo

Zaidi ya hayo, Umoja wa “RFPPN” ulishughulikia mara moja tishio kuu la kurejesha na kuhifadhi ustawi wa mazingira: ukataji miti ovyo kwa ajili ya kuni uliokuwa ukifanywa na wanavijiji wa eneo hili. Wanawake waliazimia kutafuta nishati mbadala na kuzifanya jumuiya zao ziwe na nishati ya kutosha ya kupikia.

·         Kwanza, walianzisha mtandao wa ushirika wa kusambaza kuni, mkaa na gesi ili kudhibiti matumizi na kuwasaidia wanachama wao kupata mahitaji ya kaya zao.

·         Pili, walianzisha kitalu cha miche ya miti cha kijiji na msitu wa jumuiya ili viwe vyanzo vya awali vya nishati ya kupikia.

·         Mwisho, walianzisha utaratibu wa kukusanya takataka za kila kaya na kuzirundika ili kuzuia madhara ya uchafu kwa afya za wananchi yanayotokana na utupaji ovyo wa takataka na pia kuzalisha mbolea kwa ajili ya kitalu cha miche ya miti.

Kwa kufanya hivi, wanawake sio tu walifaulu kurejesha bioanuwai na mimea ya asili ya eneo hili, bali pia juhudi zao ziliwezesha kurejesha eneoni aina mbalimbali za viumbe ambao walikuwa hawaonekani kwa miaka mingi:aina nyingi za ndege; nungunungu, nguchiro, tumbili, mbweha, ngawa, na hata paa.

Kujenga mtandao

Juhudi zao hatimaye zilifikia kiwango ambapo ustawishaji upya wa mazingira ya eneo lao usingekuwa na mafanikio bila ushiriki mpana wa vijiji vya jirani. Kwa kweli programu na mfano wa Umoja wa “RFPPN” viliongeza hamasa miongoni mwa watu wa jumuiya za jirani. Badala ya kuupanua Umoja wa “RFPPN”, wanachama wa Umoja wa Popenguine waliamua kuwatia moyo wanawake wa vijiji vya jirani kuanzisha vyama vyao na vitalu vyao vya miche, na pia taratibu na mitandao yao ya kugawa nishati ya kupikia. Hatimaye jumuiya nane zilishirikishwa na Umoja wa Popenguine chini ya kamati ya pamoja ya uratibu, na hivyo kufanya wanachama wa programu kuongezeka kutoka wale 119 wa awali hadi kufikia zaidi ya wanachama 1500. Maelfu ya miche mipya sasa huzalishwa kila mwaka na mtandao huu wa vyama.

Wakati huohuo, vikundi vya wanawake viliongeza nyanja nyingine mpya kwenye programu yao. Nyanja tatu zaidi zinazojalizana zimeongezeka kutokana na msaada wa Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya.

·         Mikopo na huduma za benki: Ili kupunguza umasikini uliokithiri uliopelekea kwenye uharibifu wa mazingira, vyama vilianzisha benki za nafaka, huduma za mikopo na ukulima mdogomdogo wa umwagiliaji wa mboga za majani katika kila kijiji. Kilimo cha mboga kilihamasisha ukusanyaji wa takataka ili kutengeneza mbolea iliyohitajika bustanini.

·         Miundombinu ya utalii na mafunzo: kutokana na watu wa Senegal nzima na hata wa nchi za nje kuvutiwa sana na majaribio ya Popenguine, wanawake waliamua kujenga miundombinu rahisi kwa ajili ya kuwahifadhi wageni wao waliowatembelea kujifunza ujuzi toka kwao. Hii ilifuatiwa na kuanzisha Kituo cha Mafunzo ya Usimamizi wa Ikolojia” (Centre for Training in Ecological Management). Sasa walipata vikundi vya wageni kutoka nchi kadhaa za kigeni ambao walivutiwa sana na mfano huu uliofaulu wa maendeleo ya ikolojia.

·         Ajira ya vijana: ili kuzuia uhamaji wa vijana wa vijana wanaohitimu shule na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wa eneo zima, vyama viliwekea mkazo maalum kuwafundisha vijana shughuli mbalimbali za kiuchumi zilizokuwa zimeanzishwa katika hifadhi hii mpya. Watu wa kujitolea kutoka vijiji na miji ya jirani wamepatiwa kazi ya kurejesha ustawi wa hifadhi na kujifunza misingi ya usimamizi mzuri wa ikolojia. Baadhi ya watu hawa wamepata ajira za kudumu. Ajira nyingi hushughulikiwa na vilabu vya vijana wa Kisenegal vinavyoshirikiana na Mfuko wa Nicolas Hulot, NGO ya Kifaransa inayoshughulikia hifadhi ya mazingira duniani kote.

Mfano wa kuigwa

Hifadhi na eneo linalolindwa sasa lina ukubwa wa zaidi ya maili 50 za mraba na hutoa fursa zaidi za maisha kwa jumuiya zinazopakana na eneo hili. Uwepo wa pamoja kati ya hifadhi ya kitaifa ya Kiafrika na wananchi majirani ni ishara ya mtindo mpya na wa matumaini wa kuhifadhi mazingira. Umoja wa “RFPPN” umeipatia Senegal na vikundi vinginevyo katika nchi za Kiafrika mfano wa usimamizi wa ikolojia uliobuniwa na wenyeji, na unaotoa faida katika muda mfupi kwa mazingira na watu wanaoishi katika mazingira hayo.

*msingi wa makala hii ni utafiti uliofanywa na watafiti wa Senegal kwa msaada na ushauri wa kiufundi wa Profesa Peter Easton wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Florida, wakishirikiana na baadhi ya jumuiya za Kiafrika. Utafiti ulifadhiliwa na Club du Sahel?OECD, CILSS na ADEA.

 

[Back to TOC]


Footer