THE WORLD BANK GROUP A World Free of Poverty
Home

[Back to TOC]

Kujua Kusoma na Kuandika na Uongozi katika Jumuiya ya Kijijini:
Uzoefu wa Nwodua, Ghana

Nwodua ni mji mdogo wenye wakazi 640 na uliopo km 20 kutoka jiji la Tamale la Kaskazini mwa Ghana, na km 3 kutoka barabara kuu ya Tamale – Kumbungu, ambayo awali ilikuwa kijia tu chenye vumbi na uchafu. Hadi mwanzoni mwa miaka ya 1980, Nwodua iliendelea, kwa kiasi kikubwa, kutengwa na biashara ya mkoa na ilikuwa na huduma chache tu za kijamii na haikuwa na shule. Barabara inayoiunganisha Nwodua na barabara kuu sasa imewekewa changarawe, na mji una maji ya bomba. Jumuiya vilevile ina kitalu cha miche ya miti, mashine mbili za kusaga unga zinazotoa chakula cha watoto wachanga, shule ya msingi, chuo cha ufundi stadi cha watu wazima, uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo na mfumo mpya wa uongozi. Mfumo huu mpya wa uongozi kusema kweli ndiyo msingi wa mafanikio mengine yote.

Mnamo mwaka 1979, mkulima mmoja asiyejua kusoma wala kuandika kutoka Nwodua aliamua kuwa wakati ulikuwa umewadia wa kuleta maendeleo ya kisasa ya Ghana kwenye jumuiya yake. Alianza kwa kumshawishi mhitimu wa shule ya kati (=elimu ya msingi) wa kijiji cha jirani kuja kuanzisha mafunzo ya kusoma na kuandika hapo Nwodua. Mafunzo yaliendeshwa kwa lugha ya kuzaliwa ya hapo Nwodua, jambo ambalo halikuwaridhisha vijana wengi waliojiunga na programu hiyo. Wao walihitaji Kiingereza, na hivyo wakaacha kusoma. Lakini yule mkulima aliyekuwa anaendesha programu hii pamoja na rafiki yake waliendelea na masomo, wakimlipa mwalimu kwa kufanya kazi kwenye mashamba yake pale waliposhindwa kumlipa mshahara wake kwa fedha taslimu.

Kufanya mafunzo ya kusoma na kuandika yatekelezeke

Baada ya muda mfupi kupita mwalimu wa kwanza aliondoka na kujiunga na Chuo cha Ualimu ili apate kazi nzuri zaidi. Wanafunzi wake wawili aliowaacha walimwajiri mwalimu mwingine na wakati huohuo wakawashawishi baadhi ya wanafunzi waliokuwa wamesusa masomo awali kurejea masomoni. Kisha walitumia mafanikio haya ya wastani kuushawishi Uaskofu wa Kanisa Katoliki kuanzisha shule ya msingi hapo Nwodua kunako mwaka 1984. Miaka miwili baadaye, wanafunzi wote wawili walifaulu mtihani wa kitaifa wa kusoma na kuandika na hivyo kuwa na sifa ya kuanzisha vituo vyao vya mafunzo ya kusoma na kuandika katika vijiji vya jirani.

Mafanikio katika juhudi zao yaliwaongezea majukumu na fursa. Wote wawili walichaguliwa kuwa wasimamizi wa ugani na Mradi wa Mafunzo ya Kusoma na Kuandika wa Dagbani, ambao ulikuwa ndio tu umeanzishwa, na baada ya muda mfupi madarasa sabini na sita yalikuwa yakiendeshwa mkoani kote. Kutokana na nafasi yake kama makao makuu ya mkoa ya mafunzo ya kusoma na kuandika Nwondua ilifungua Shule ya Msingi ya Watu Wazima mnamo mwaka 1989 ambako zaidi ya wakazi hamsini wa jumuiya walifuzu mwaka uliofuata na kupata vyeti vya kumaliza elimu ya msingi. Baadhi yao waliendelea na elimu ya sekondari. Wakati huo huo, mafunzo ya kusoma na kuandika yakafanywa msingi wa programu nyingi za maendeleo ya jumuiya.

Miongoni mwa programu hizo, ya kwanza ilikuwa uanzishaji wa Kamati ya Afya ya Msingi, ambayo ilipeleka timu ya wakazi kwa ajili ya mafunzo kwenye Huduma ya Afya ya Taifa huko Tamale na baada ya hapo ikafadhili kampeni ya kukomesha utapiamlo na kifafa na dege la watoto. Juhudi hizi zilizingatiwa na UNICEF, ambayo iliisaidia Kamati kununua mashine ya kusaga nafaka ili kutayarisha chakula cha kulikiza watoto wachanga. Wakati huo huo Kamati ilihakikisha kwamba fedha zilizotokana na kuazimisha mashine hii na pia mauzo ya bidhaa zilizosagwa zilitumika kununulia mashine ya pili, na hivyo kuifanya jumuiya kuwa na kiwanda endelevu cha kusaga nafaka.

Kuhifadhi upya mazingira

Programu iliyofuata ilikuwa katika eneo la kilimo mseto na, kama ile ya mwanzo, ilitokana na mafunzo yaliyotolewa kwenye vituo vya kusoma na kuandika na vya Elimu ya Watu Wazima. Washiriki watano walihudhuria mafunzo yaliyofadhiliwa na UNDP (Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo) mjini Tamale juu ya matatizo ya kuenea kwa jangwa huko Ghana ya Kaskazini na jinsi jumuiya za huko zinavyopaswa kupambana na janga hilo kwa kupanda miti upya. Waliporejea Nwodua waliwashawishi wakazi wenzao wengi kuanzisha vitalu vya miche ya miti. Ingawa matayarisho yote ya msingi yalikuwa yamekamilika ilipofika mwaka 1991 na 1992, ilidhihirika punde kuwa programu hii isingefanikiwa kutokana na ukame. Mafanikio yake yalitegemea upatikanaji wa njia mbadala ya kuleta maji mengi kwenye jumuiya.

Klabu ya Wakulima Vijana Nwodua ilisaidiwa na uongozi wa Mradi wa Mafunzo ya Kusoma na Kuandika wa Dagbani kuiomba UNDP ifadhili utandazaji wa mabomba ya maji kutoka kwenye mabomba yaliyokuwa yanapeleka maji Tamale hadi Nwodua, umbali wa Takribani km 5. UNDP ilikubali kutoa ufadhili na wanakijiji wakachimba mfereji wa km 5 kwa ajili ya kutandazia mabomba. Mradi ulifanikiwa na Kamati ya Maji ya Nwodua inamudu kulipia ada za kila mwezi kwa Tume ya Maji Machafu kwa kuitoza ada ya maji kila kaya kijijini inayotumia maji hayo. Wakati huohuo, upatikanaji wa maji umeondoa tatizo lililokuwa likizikabili juhudi za uendelezaji wa vitalu vya miche na za upandaji miti upya za Nwodua. Kitalu kilianza kugawa miche ya miti mbalimbali ya kibiashara na vivuli bure kwa wakazi wa Nwodua, na kuwauzia watu wa nje ya Nwodua. Mwaka 1995, kwa mfano, zaidi ya miche pandikizi 2000 ya miembe na miche 4000 ya mikorosho iligawiwa kwa vikundi na watu binafsi katika mkoa wote wa jirani, ikiwa ni pamoja na vyombo kama Baraza la Wilaya Ndogo ya Kumbungu. Kitalu hivi sasa kina mfuko wa mtaji unaozidi kukua kwa ajili ya kuanzisha miradi mingine mipya.

Biashara hii iliyopanuka na maeneo ya nje ililazimisha kuboresha barabara ndogo inayotoka Nwodua kuelekea kwenye barabara kuu ya Tamale. Kamti ya Barabara iliundwa mwaka 1991 na mwaka uliofuata viongozi wa Benki ya Dunia walikuwa wameombwa na kushawishika kusaidia uimarishaji wa barabara hiyo yenye urefu wa km 3, mradi tu kwamba kijiji kingetoa nguvukazi pamoja na malazi ya wataalam wa ujenzi na mafundi sanifu waliokuwa wakishiriki kazi ya ujenzi wa barabara hiyo. Barabara ilikamilika kujengwa mwaka uliofuata na Kamati ya Barabara ikapewa jukumu la kuitunza na kupanga mipango ya kuziboresha barabara za kuingilia kwenye barabara hiyo iliyokwishajengwa.

Kuanza na watu wazima

Urahisi wa kusafirisha mazao nje ya Nwodua ulimaanisha kuwa ilikuwa rahisi vilevile kufika Nwodua, na jumuiya ikaanza kwa namna mbalimbali kuwa kitovu cha stadi mbalimbali kwa mkoa wa jirani. Stadi ya nyongeza ulikuwa uanzishwaji wa kituo cha ufundi sanifu mnamo mwaka 1999 kilichofadhiliwa na Denmark. Kwa kujengwa kituo hicho, kijiji sasa kilikuwa na vituo kadhaa vya fursa za kielimu – vitatu kwa ajili ya watu wazima (Kituo cha Mafunzo ya Kusoma na Kuandika, Shule ya Msingi ya Watu Wazima na Kituo cha Ufundi Sanifu) vikiwa pembeni mwa shule ya msingi kwa ajili ya watoto.

Kamati za Maendeleo za Nwodua mara nyingi huulizwa kwa nini mipango yao ya elimu hadi sasa imekuwa ikiwazingatia zaidi watu wazima kuliko watoto. Jibu lao ni rahisi tu: Ndiyo njia iliyo bora zaidi kwa vijiji vilivyokuwa awali masikini sana kama hiki chetu. Iwapo watu wazima wengi zaidi watakumbana na fursa mpya na kujifunza jinsi ya kufaidika nazo, basi wengi wao watakuwa na shauku ya kuwapeleka watoto wao kwenye shule za msingi.

Uongozi bora mpya ndiyo kiini

Pamoja na mafanikio ya juhudi hizi mbalimbali siri ya maendeleo mapya ya Nwodua iko katika kiini cha maendeleo hayo – uongozi bora mpya wa jumuiya uliobuniwa polepole na mamlaka ya kijiji kwa kushirikiana na vijana. Uongozi huu ndio unaosimamia na kuendeleza miradi ya uzalishaji ya wanakijiji. Viongozi wa mwanzoni wa programu ya mafunzo ya kusoma na kuandika waliafikiana na chifu wa kijadi wa Nwodua pamoja na baraza lake kuanzisha Kamati Kuu ya Maendeleo iliyopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji mzuri wa miradi na uhifadhi wa masilahi yao. Kamati hii, kwa upande wake, imeanzisha kamati nyingine ndogondogo zinazosimamia kila sekta ya maendeleo ya jumuiya na kutoa ripoti kwa Kamati Kuu. Kamati iko chini ya uenyekiti wa mkulima mmoja mwenye umri wa miaka sitini na mitano, mwenye kuheshimika katika jumuiya, ingawa hajui kusoma wala kuandika. Lakini kati ya wajumbe wengine wanane wa kamati hiyo, ni mmoja tu ana umri wa zaidi ya miaka arobaini na tano, na saba ni wahitimu wa mafunzo ya kufuta ujinga au madarasa ya shule ya msingi ya watu wazima.

Kamati Kuu hufanya kazi kupitia kamati nane za kisekta, kila moja ikishughulikia sekta moja mahususi. Sekta hizo ni: mafunzo ya kusoma na kuandika ya watu wazima, utunzaji wa afya ya msingi, usagishaji na usindikaji wa vyakula, kilimo mseto, ufundi stadi na sanifu, mafunzo ya kilimo na ujenzi/utunzaji wa barabara. Katika kuandaa mfumo huu wa usimamizi, mambo mawili yamejitokeza. Kwanza, uangalizi na ufadhili uliopo unaifanya miradi kuwa na uendelevu wenye uhakika. Pili, hatua kwa hatua, Kamati Kuu ya Maendeleo imekuwa serikali tendaji ya kijiji hapo Nwodua – lakini sio serikali ya hadhi tu – na imefaulu kutoa fursa kwa watu kubuni miradi ya maendeleo na kusaidia utoaji wa huduma bora za kijamii.

Hata hivyo mafanikio ya Kamati Kuu ya Maendeleo yanatokana na sababu nyingine mbili – kwa upande mmoja, hamasa kubwa ya mabadiliko iliyoletwa na mfululizo wa mafunzo ya watu wazima na elimu isiyo rasmi yaliyotolewa kijijini na maeneo ya jirani ya kijiji; na, kwa upande mwingine, msukumo uliotolewa na wakazi wawili ambao awali hawakujua kusoma wala kuandika, walianzisha harakati za kuleta maendeleo haya takribani miaka ishirini iliyopita na wakakataa vipingamizi vyovyote kuwashinda. Ari ya watu binafsi na kuendelea kupatikana kwa mafunzo mapya na fursa ya kuyatumia kulichochea mafanikio katika maendeleo ya jamii ambayo yalidhaniwa hayawezekani miaka ishirini iliyopita. Lakini uvumbuzi wa uongozi bora mpya wa jumuiya ndiyo ulikuwa msingi uliowezesha kupatikana kwa mafanikio yote haya.

*Msingi wa makala hii ni utafiti uliofanywa na watafiti kutoka Ghana, Canada na Marekani kwa msaada na usimamizi wa kiufundi wa Prof. Peter Easton wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Florida. Utafiti ulifadhiliwa na Club du Sahel/OECD, CILSS na ADEA.

 

[Back to TOC]


Footer