|
WAENDESHA
BENKI ZA VIJIJI: UZOEFU WA FANDENE (SENEGAL) Fandene yenyewe ni matokeo ya maingiliano ya kihistoria
kati ya mbari za Kiserere na Kiwolof. Kijiji hiki kwa kiwango
kikubwa ni cha Kikristo na kwa miaka mingi kilikaliwa na wamisionari
wa Kikatoliki na kuwa kituo kikuu cha jumuiya, lakini huchangia
rasilimali chache za bonde la jirani na kingo za msimu za mto
na jumuiya za Kiislam kadhaa mbalimbali. Hatua za hivi karibuni
zilizochukuliwa na wenyeji kwa kiwango fulani zinatokana na mtazamo
wa wahamiaji kutoka Fandene dhidi ya kiwewe cha ukame mkuu wa
Saheli cha mwanzoni mwa miaka ya 1970. Katika juhudi za kuwasaidia
wanajumuiya wa nyumbani kwao kupata ufumbuzi wa tatizo lililokuwa
linawakabili na kukwepa jumuiya isitoweke, vijana waliokuwa wamekwenda
kusoma shule ama kufanya kazi, walishiriki kuunda Chama cha Vijana
wa Fandene (“Association des Jeunes de Fandene – AJF) mnamo mwaka
1972. Kutoka
Utamaduni hadi Kilimo
Kwa miaka kumi na mitano ya kwanza ya uhai wake, AJF
ilijishughulisha zaidi na kufadhili matukio ya kiutamaduni yaliyolenga
kuwahamasisha vijana waikumbatie ama wairejelee jumuiya yao ya
nyumbani, na wakati huohuo warejeshewe utambulisho wao wa kiutamaduni.
Miradi ya maendeleo ilipewa uzito mdogo, lakini hata hivyo shughuli
za AJF ziliwafanya baadhi ya wasomi vijana kurejea kuishi kijijini
tena na hivyo kuunda kikundi kipya cha wakulima wa “kisasa” na
wenye mtazamo wa kihakiki. Polepole kikundi hiki hakikuridhika
na programu ya AJF kujibana na matukio ya kiutamaduni tu na kuongozwa
na watu wa kutoka nje. Hivyo, kunako mwaka 1987, Chama kilichukua msimamo
mpya. Katika kukabiliana na upungufu wa muda mrefu wa chakula
eneoni, wanachama wa AJF walianza kufanya utafiti wakishirikiana
na wanajumuiya za jirani ili kulielewa vema zaidi tatizo lao na
kulipatia ufumbuzi unaowezekana. Utafiti huu ulikuwa na matokeo
matatu muhimu: ·
Watafiti
waliabaini kuwa hatua kadhaa zilikuwa tayari zimeanza kuchukuliwa
na wakulima wadogowadogo wenyewe – hatua zilizokuwa na nafasi
kubwa ya kupanua uchumi wa wenyeji wa kuboresha msingi wa maliasili,
lakini hatua ambazo zilikuwa zikikwamishwa na upungufu wa mikopo
na mitaji ya kuiendeleza. ·
Ukosefu
wa huduma za mikopo kwa kiasi kikubwa ulitokana na ukosefu wa
dhamana za mikopo na chombo ambacho kingewadhamini wakulima wadogowadogo. ·
Wakati
huohuo, wanachama wa AJF walichunguza hali na utendaji kazi wa
miradi ya hivi karibuni ya eneoni iliyokuwa ikifadhiliwa na mashirika
yasiyo ya kiserikali (NGOs), na kubaini kuwa mingi ya miradi hiyo
haikufanikiwa kwa vile ilibuniwa nje na haikuendana na juhudi
zilizopo za wananchi. Kutatua
tatizo la mikopo
Uamuzi ulikuwa kukabiliana na matatizo haya kwa kuanzisha
namna fulani ya chombo cha kuweka na kukopa fedha kisicho rasmi.
Mwanzo ulikuwa wa kiwango cha chini: kila mwanachama wa AJF alichangia
FCFA 250 (takribani $ 1 ya wakati huo) kwenye mfuko wa pamoja
na mfuko huo ukaanza kutoa mikopo midogomidogo kwa wanakijiji
kwenye miradi inayofaa. Wakopaji walilipa riba ya asilimia 15
kwa mwaka, huku wakitafuta njia nyingine za kuongeza mitaji yao.
Mojawapo ya njia hizo ilikuwa kupanua uanachama wa mfuko hadi
kwa jumuiya za jirani. Kazi hii haikuwa ngumu. Vijiji vya jirani
viliihitaji sana huduma hii na hivyo vyenyewe vilikuwa na shauku
kubwa ya kutaka kujiunga na mfuko. Kwa njia hii, mtandao wa ushirika wa kuweka na kukopa
fedha polepole ulisambaa kwenye jumuiya zote 34 za eneo la Fandene
na kuwa na muundo imara zaidi. Kila tawi la ushirika – jumla ya
matawi 19 – lilikuwa na kitengo cha wanawake na kitengo cha wanaume,
na viongozi wa kila kitengo walipatiwa mafunzo ya uhasibu, kutathmini
thamani ya mikopo na uendeshaji wa mikopo. Wakazi wa jumuiya zilizochangia
kwenye mfuko walishawishiwa kuomba mikopo kwa maandishi kupitia
maofisa wao wa vitengo, na uongozi wa ushirika polepole ulijifunza
kufanya upembuzi yakinifu wa mikopo iliyoombwa na kuwapatia wakopaji
msaada wa kiufundi katika kuhakikisha kuwa mikopo yao ingelipishika.
Hatimaye timu ya watathmini iliundwa ili kuzisaidia kamati za
wenyeji za kuweka na kukopa fedha kujifunza mbinu za kutathmini
maombi ya mikopo na za kukabiliana na mahitaji ya kiufundi ya
wafanyabiashara wadogowadogo. Kusaidia
uvumbuzi mpya wa kiuchumi wa wenyeji
Ushirika
uliopanuka zaidi wa kuweka na kukopa fedha uliwekea mkazo maalum
katika kuwasaidia wakulima na wafanya biashara ndogondogo kuvumbua
mikabala mipya ya kuimarisha kilimo na uuzaji wa mazao yao. Ifuatayo
ni mifano ya mambo yaliyotekelezwa na ushirika katika miaka mitano
ya kwanza ya uhai wake: ·
Vikundi
vya uzalishaji vya wanawake vilisaidiwa kubuni mbinu za uuzaji
bidhaa zilizowakwepa walanguzi, na hivyo kuwawezesha wanawake
kuuza matunda-mwitu (“bissap fruits”) kutoka misitu ya jirani
na vikapu vya kienyeji moja kwa moja kwenye soko la Dakar na pia
kwenye vyama vingine vya vijiji eneoni. Hadi kufikia mwaka 1995
vikapu elfu moja vilizalishwa kila wiki kwa mtindo huu. ·
Chama
cha AJF kilitoa mikopo kwa wakulima waliotaka kurejesha tena kilimo
na mauzo ya mihogo eneoni na waliotaka kupanua upandaji na matumizi
ya kunde. ·
Mikopo
ilitolewa kwa vikundi vya wanawake ili kuanzisha ushirika wa utengenezaji
sabuni na mauzo yake. ·
Mashirika
ya kuweka na kukopa fedha yalitoa mikopo mingi kwa ajili ya kuchimba
visima, uendelezaji wa bustani za kumwagilia na uuzaji wa mazao
ya bustani hizo. Kadiri shughuli na mtaji vilivyoongezeka, ndivyo ukubwa
na idadi ya mikopo vilivyoongezeka pia. Kwa kipindi cha miaka
mitano ya kwanza, wastani wa matumizi ya fedha katika sekta mbalimbali
ulikuwa kama ifuatavyo: Maendeleo ya mifugo na soko lake – FCFA 5,600,000 Viwanda na biashara ndogondogo - FCFA 2,800,000 Kilimo bora - FCFA 500,000 Uchimbaji
visima
-
FCFA 500,000 Faida za mwaka kutokana na uendeshaji wa mikopo zilipanda
pia kutoka chini ya FCFA 100,000 mwaka 1991 hadi kufikia zaidi
ya 700,000 kunako mwaka 1994 na ilipofikia mwaka 1998 mtaji wa
chama cha kuweka na kukopa fedha kilichounganisha vijiji kadhaa
pamoja uliongezeka hadi kufikia zaidi ya FCFA milioni 30,
au takribani $ 60,000. Kusuka
mfumo mpya wa kijamii na kiuchumi
Hata hivyo, matokeo yaliyokuwa muhimu zaidi ya shughuli hizi ni ujenzi wa ushirika na
muunganisho wa jumuiya za Kisenegal zenye mbari (makabila) zinazotofautiana.
Vijiji 34 vya Fandene vinajumuisha Wakristo, Waislamu na waumini
wa dini za kienyeji na vina mchanganyiko wa makabila (Waserere,
Wawolof, Wabambara, Wafulani…). Lakini licha ya mchanganyiko huu,
watu hawa wameshirikiana vema kuanzisha vyombo vya kuweka na kukopa
fedha na pia katika kuviendesha. Vitengo vya wanawake na wanaume
vya chama cha AJF daima vimekuwa na nguvu na uzito ulio sawa. Licha ya hayo, chama kimeanzisha mipango ya uuzaji
wa mazao na vyama vya ushirika vya wakulima wadogowadogo katika
maeneo mengine ya Senegal ambako bidhaa nyingi za wanachama huuzwa
huku nao wakinunua mahitaji yao kutoka kwa wakulima hao. Jambo
muhimu zaidi ni kwamba chama cha Fandene kimeanzisha timu za kiufundi
ili kuvisaidia vikundi vichanga na visivyo na uwezo wa kifedha
vya jirani na jiji la Thies na mji mkuu wa taifa, Dakar, ambavyo
vinahitaji kuanzisha programu zao za kuweka na kukopa fedha. Kwa
hali hii msaada wa kiufundi sasa unatoka vijijini na kupelekwa
mijini! |