THE WORLD BANK GROUP A World Free of Poverty
Home

[Back to TOC]

Wanawake wa Senegal Wajenga Upya Utammaduni Wao

Kwa miongo mingi makao makuu ya Utawala wa Kifaransa huko Afrika Magharibi, yaani nchi ya Senegal, kama zilivyo nchi nyingine za Sahel, wakazi wake wengi wanaendelea kuishi vijijini. Ingawa asilimia 62 ya watu huishi vijijini, hata hivyo zaidi ya asilimia 85 ya utajiri wa nchi iko mijini. Kama ilivyo kwa nchi nyingi, wanawake na wasichana ndio walio katika hali ngumu zaidi. Mwaka 1995, kiwango cha kujua kusoma na kuandika cha wanawake kitaifa kilikuwa karibu nusu ya kile cha wanaume (asilimia 23 ikilinganishwa na asilimia 44), na tofauti ilikuwa kubwa zaidi huko vijijini.

TOSTAN, inayomaanisha “kujitoa kutoka katika yai” katika Kiwolof, lugha inayozungumzwa na idadi kubwa zaidi ya wananchi milioni 7.9 wa Senegal, ni miongoni mwa mipango kadhaa ya kielimu ya maendeleo ya vijijini na ya wanawake inayoshughulikia matatizo kwenye machimbuko yake. Mpango hutoa programu ya mafunzo ya miezi 18 inayojumuisha elimu ya msingi kwa lugha za kitaifa inayozingatia masuala halisi ya kimaendeleo, na huwapatia wanavijiji rasilimali za kuboresha hali zao za maisha huku wakizidi kujiamini katika kukabiliana na maisha yao. Licha ya kujua kusoma na kuandika, programu hii kamambe huwapatia washiriki zana za kushughulikia masuala ya kijamii kama vile afya, usafi wa mazingira.

Mpango hutumia viunzi sita vinavyounganisha ujuzi wa kusoma na kuandika na stadi za maisha katika utaratibu shirikishi wa kutatua matatizo. TOSTAN imefaulu kuendeleza mfungamano kati ya elimu ya msingi na maendeleo ya vijijini, ikiwapatia watu wazima wanaosoma sio tu ujuzi na kusoma, kuandika na kuhesabu katika lugha zao za kitaifa, bali mbinu za kuyaelewa na kuyatatua matatizo yao.

Miaka kadhaa iliyopita, shirika lisilo la kiserikali la TOSTAN liliitikia maombi ya viongozi wa kijiji cha Malicounda ambao walikuwa wameshaona athari za programu zake za mafunzo kwa wanawake katika jumuiya za jirani na kuisaidia jumuiya hii ya Wabambara wa Senegal ya Kati Magharibi kuanzisha kituo chake. Programu ilitilia mkazo maalum juu ya utambuaji na utatuzi wa matatizo ya kawaida, na kimoja kati ya viunzi vya mwisho vya mafunzo kilishughulikia suala la afya ya wanawake na ngono. Programu hii ilivunja rekodi kwa kuungwa mkono mno na wanawake wa vijijini. Mara tu baada ya kumaliza mafunzo yao, wanawake waliojua kusoma na kuandika wa Malicounda waliamua kulishughulikia suala la kijadi la tohara ya wanawake – utamaduni wa siku nyingi wa jumuiya za Wabambara/ Wamandigue na Wapulaar. Wakitumia uzoefu wa maeneo mengine na athari za tohara kwa afya ya wasichana na maisha yao ya kingono, waliandaa hoja nyingi ambazo hatimaye zililifanya baraza la kijiji kufuta rasmi desturi ya kufanya tohara. Wakati wa miezi ya Mei hadi Julai 1997 – kipindi cha kawaida cha kutahiri wasichana wadogo – tohara hazikufanyika Malicounda kwa mara ya kwanza katika historia ya jumuiya hiyo.

TOSTAN na UNICEF ziliwaunga mkono wanawake kwa kuandaa ziara ya waandishi wa habari ishirini wa Kisenegal waliowatembelea na kuwauliza maswali juu ya msimamo wao. Wanawake waliwafanyia wageni wao igizo kuwaonyesha sababu za kufikia uamuzi huo na hoja walizozitumia kuwashawishi wanakijiji wengine. Ziara hii ililitangaza sana suala hili, lakini pia ilizua maoni ya vitisho na kukosolewa kutoka jumuiya jirani za kabila la Malicounda. Wakiwa wamehuzunika lakini bila kutishika, wanawake wa kikundi  cha Malicounda waliamua kuandaa ujumbe kwenda kwenye vijiji viwili vya jirani kuwashawishi wanawake wa huko juu ya umuhimu wa uamuzi wao wa kukomesha ukeketaji wa viungo vya kike.

Katika moja ya jumuiya hizo – jumuiya ya Wangerin Bambara – wanawake waliohitimu punde tu programu ya TOSTAN waliamua kukiidhinisha “kiapo cha Malicounda”. Rais wa Chama chao cha wanawake, mwenyewe binti wa ngariba, alisema kwamba binti yake alitokwa na damu nyingi sana alipotahiriwa, na hivyo wakati wa kubadili mila hii ulikuwa umewadia.

Wakazi wa jumuiya ya pili, Waker Simbara, walimua kwamba wasingeweza kuifuta mila hii bila kushauriana na wanakabila wenzao wa vijiji vya jirani. Hivyo kwa kipindi cha majuma manane, wanaume wawili ambao walikwisha shiriki katika programu za TOSTAN – mmoja mwezeshaji wa TOSTAN na mwingine Imam wa Msikiti mwenye umri wa miaka 66 (kiongozi mwandamizi wa Kiislam) – walizuru kijiji kimoja baada ya kingine kujadili na wananchi madhara ya tohara kwa wanawake. Awali wanaume hawa walidhani kuwa wangefukuzwa katika jumuiya nyingi. Badala yake waligundua kuwa taarifa za Malicounda zilifungua milango na nyoyo, na wakasikia maelezo ya kutisha toka kwa wanawake, wakielezea kwa mara ya kwanza juu ya uzoefu wao.

Wanaume hawa wawili walirejea wakiwa wameshawishika juu ya umuhimu wa kile walichosikia na kile walichokuwa wakikifanya. Waliwasaidia wanawake wa Malicounda, Ngerin na Ker Simbara kuandaa mkutano wa vijiji vyote huko Diabougou. Mnamo Februari 1998, wawakilishi watatu – chifu wa kijiji na wawakilishi wawili wa kike – kutoka vijiji kumi na vitatu walikutana kwa siku mbili kujadili tatizo la tohara na wakaunda “Azimio la Diabougou”, lililowataka wanavijiji 8,000 kusimamisha mara moja tohara kwa wasichana.

Taarifa za mkutano huu zililifikia eneo la Casamance la Senegal ya Kusini, ambako kikundi kingine cha vijiji – vyote vya Wapulaar, kabila linalotahiri asilimia 88 ya wasichana – kilifanya mkutanno na maazimio kama yale ya Diabougou. Mkutano wao ulihudhuriwa na wawakilishi kutoka jumuiya 18, na wafanyakazi wa sekta ya afya na Imam aliyeheshimika sana wa Medina Cherif, aliyewahakikishia wanawake kwamba dini ya Kiislamu haihitaji wasichana watahiriwe na inawahakikishia wanawake haki ya afya na hadhi ya utu. Wanawake wengi walielezea madhara yanayoletwa na tohara. Mmoja alieleza kwa masikitiko juu ya vifo vya binti zake wawili waliopoteza maisha baada ya kutahiriwa; na ngariba alikiri kuwa kuna msichana aliyekufa kijijini kwake mwaka jana. Wanawake wengine walizungumzia juu ya matatizo wakati wa kujifungua na juu ya maumivu wakati wa kujamiana. Kikundi kilihitimisha mkutano wake kwa kutoa azimio lililokana tohara.

Mpango huu umeendelea kupanuka. Mapema ulipoanza, Rais Abdou Diouf wa Senegal mwenyewe alipendekeza “ Kiapo cha Malicounda” uwe mfano wa kuigwa na taifa zima. Mara tu baada ya mikutano ya Casamance, wanawake wa eneo la St. Louis la Senegal wanaandaa sasa mkutano wa vijiji vyao, utakaofanyika Februari 1999.

Utaratibu wa “ Mafunzo tendaji” unaoendeshwa miongoni mwa wanawake na mpango wa TOSTAN nchini Senegal unaelekea kuleta mabadiliko makubwa ya kiutamaduni. Mambo yanayochangia kwenye mafanikio ya mpango wa TOSTAN wa elimu na maendeleo endelevu yanajadiliwa zaidi hapa nchini.

Hoja

MIZIZI YA UTAMADUNI. Pamoja na utumiaji wa lugha za kitaifa, kuthamini kwa kiwango kikubwa utamaduni wa Kiafrika ndio msingi wa mpango wa elimu wa TOSTAN, unaoonyesha mfungamano wa kiutendaji baina ya utamaduni na elimu.

LUGHA ZA KITAIFA.Ingawa Kifaransa ndio lugha rasmi ya Senegal, serikali imezidi kuhimiza matumizi ya lugha za kitaifa katika programu za kujifunza kusoma na kuandika, kwa vile inatambua kuwa mafunzo huwa mepesi zaidi mtu anapotumia lugha yake ya kuzaliwa. Aidha uelewa wa lugha ya kuzaliwa huweza kuwa ni msingi mzuri wa kujifunza lugha za kimataifa. Kujifunza kwa kutumia lugha ya kuzaliwa huleta heshima na fahari, huwapa wanawake uwezo wa kuelezea mambo yao majumbani mwao na katika jumuiya zao; huwafanya watu wajivunie mahali waishipo, na hivyo kuwapa moyo wanaume kuwekeza mitaji kwenye jumuiya yao badala ya kuhamia mijini. Hali kadhalika, huondoa hali ya kutengwa vijijini wanayihisi watoto walioelimishwa kwa Kifaransa tu, na hivyo kuleta mawasiliano na mshikamano miongoni mwa wanachi wa marika mbalimbali.

Mhimili wa programu ni UTATUZI WA MATATIZO, na kutoa motisha kubwa ya kujifunza kusoma na kuandika. Stadi zinazofundishwa kwenye programu hii yenye hatua tano ni pamoja na (i) utambuzi na uchambuzi wa tatizo; (ii) kuchunguza masuluhisho ya tatizo kwa kuzingatia fedha, vifaa, nguvukazi na muda uliopo;  (iii) kupanga suluhisho: kipi kinahitaji kutimizwa? Ni lini hatua zinapaswa kukamilika? Nani mwenye dhamana ya kufanya hivyo? Nguvukazi ipi , vifaa gani, na fedha kiasi gani zinahitajika? Vipingamizi gani vyaweza kujitokeza? (iv) utekelezaji wa suluhisho; na (v) tathmini ya matokeo: Je, tumelitatua tatizo?

USHIRIKI. Mpango wa TOSTAN ulibuniwa na wanavijiji ukiwashirikisha kwa kiwango cha juu kabisa kwa kipindi cha miaka kumi. Msingi wa mitaala ya mafunzo ni hadithi, methali, nyimbo na mila za kila mahali zilizokusanywa kwa kutembelea kila kijiji na kusikiliza na kurekodi mapokeo simulizi. Mbinu za kufundishia ni shirikishi na mara nyingi wanafunzi huzishirikisha familia zao na jumuiya katika harakati za kutatua matatizo.

WANAWAKE. Wanawake ndio wenye kiwango cha chini kabisa cha elimu nchini Senegal, kiwango chao cha kujua kusoma na kuanduka kikiwa ni asilimia 74.9 mwaka 1990. Wanawake hususan wamekuwa wakifaidika sana na mkabala wa lugha kamili wa TOSTAN ambao huanza na uzoefu halisi wa maisha ya kawaida ya kila siku badala ya udhahania. TOSTAN kimekuwa kituo cha mafunzo ya viongozi kwani wanawake wanapata kujiamini, wanaanza kutambua matatizo kama vile ya upatikanaji wa maji, na waanza kuleta mabadiliko katika jumuiya zao. Pamoja na hayo, wanaume hawajatengwa: takribani theluthi moja ya washiriki ni wanaume, na – kama mfano wa Ker Simbara unavyoonyesha – wanaweza kuchukua hatua nyingi muhimu za kupunguza kero zinazowakabili wanawake.

Namna ya kuandaa Mikabala

Licha ya njia ya ushirikishwaji iliyotajwa awali, wanafunzi pia walihusishwa katika uandaaji wa maudhui ya programu kwa kutumia mbinu ya majaribio, mazungumzo na uangalizi wa jinsi maazimio yalivyotekelezwa. Mwanzoni njia hii ilikuwa ya gharama kubwa lakini hatimaye ilionekana kuwa ni ya nafuu kutokana na kuigwa kwa mafanikio na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali (NGO). Brosha ya UNESCO kuhusu TOSTAN inaeleza kuwa elimu ya msingi “hukumbusha mengi katika maisha ya watu kuliko mradi wa kawaida wa mafunzo ya kusoma na kuandika…. Uelewa wa jinsi kila kiunzi kitakavyochangia kubadili maisha na mazingira yao ni motisha yenye nguvu sana kwa wanafunzi”. Namna ya utatuzi wa matatizo ndio msingi wa mkabala wa TOSTAN na huweza kurekebishwa kwa urahisi katika mazingira tofauti tofauti.

Matatizo Yaliyokuwepo

Mwaka 1987 hapakuwepo na programu zozote za elimu ya msingi katika lugha za kitaifa nchini Senegal, na Wizara mbili za serikali zilishughulikia mafunzo ya kusoma na kuandika lakini aghalabu bila ya mafanikio. Programu zilizokuwepo zilihusiana kidogo sana na maisha halisi na zilipelekwa kwa watu wasiojua kusoma na kuandika, ambako stadi zilizofundishwa na kutotumika kihalisi zilisahaulika baada ya muda mfupi. Programu ya elimu ya msingi ya TOSTAN ilishughulikia tatizo jingine la msingi, uchoshi, kwa kuhusisha elimu na maisha binafsi  na ya jumuiya na kuandaa vifaa vya mafunzo vinavyovutia vinavyotokana na mazingira ya wanafunzi – lengwa. Awali kupata wawezeshaji wa programu haikuwa rahisi, na washiriki hawakupenda kulipia gharama za wawezeshaji wao wenyewe. Walipendelea kutumia fedha zao kugharamia vifaa vya mafunzo au ujenzi wa madarasa. Wahitimu wa TOSTAN ndio sasa wamepatiwa mafunzo ya kuwa wawezeshaji na ndio wanaofanya idadi kubwa ya wafanyakazi wa TOSTAN.

Masuluhisho na Mahitimisho

Stadi za kutatua matatizo zinazotolewa kwenye kiunzi cha kwanza ndizo hutumiwa kwenye viunzi vyote vingine, vinavyoshughulikia: mambo ya usafi, uongezaji maji chumvi mwilini na chanjo, stadi za usimamizi wa fedha na vifaa, usimamizi wa nguvukazi, uchunguzi wa hali halisi na miradi ya kuzalisha mapato. Kwa kutumia stadi hizi, washiriki wanawake wameanzisha miradi kadha midogo midogo ya uzalishaji mali. Mbinu za TOSTAN vilevile zimetumika kuwanufaisha watoto walioko nje ya shule kwa kuwaandalia mtaala unaojumuisha kusoma, kuandika, hesabu, utatuzi wa matatizo, afya na usafi, lishe, uongozi wa familia, haki za watoto, historia, jiografia, elimu ya amani, stadi za uongozi na dinamiki (nguvu) za vikundi. Kwa kutumia mkabala shirikishi, vijana (watoto waliobalehe) hujifunza kutoa matini zao wenyewe.

Kipeperushi cha UNESCO kuhusu TOSTAN kimetoa hitimisho linalofaa: “kuwepo kwa programu kamambe inayowapatia washiriki zana za kutatua matatizo na inayoshughulikia matatizo muhimu ya afya, usafi, na mazingira ni jambo lenye manufaa kwa maeneo mengi ya Afrika yanayokabiliwa na viwango vikubwa vya ujinga, hasa miongoni mwa wanawake. Mkazo zaidi wapaswa kuwekwa juu ya utekelezaji wa programu hizi zilizochunguzwa na kujaribiwa vema badala ya kubuni programu mpya… TOSTAN imeonyesha kuwa watu wasio na elimu yoyote rasmi, kutoka vijiji vyenye rasilimali chache kabisa, wanaweza kuboresha maisha na mazingira yao kupitia programu imara, na hivyo kuwa huru na kujitegemea zaidi”.

*Msingi wa makala hii ni utafiti uliofanywa na watafiti wa Senegal kwa msaada na ushauri wa kiufundi wa Prof. Peter Easton wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Florida, wakishirikiana na baadhi ya jumuiya za Kiafrika. Utafiti ulifadhiliwa na Club du Sahel/OECD, CILSS na ADEA.

 

[Back to TOC]


Footer