THE WORLD BANK GROUP A World Free of Poverty
Home

[Back to TOC]

MIFUMO YA MAARIFA YA ASILI ENDELEVU KATIKA KILIMO KWENYE MAENEO YA VIJIJINI YA MAJIMBO YA KASKAZINI NA KUSINI YA MATABELELAND NCHINI ZIMBABWE

 Uchunguzi Kifani wa Zimbabwe

Utafiti huu ulichunguza Mifumo ya Maarifa ya Asili katika kilimo kwenye maeneo ya vijijini ya nchini Zimbabwe, ukilenga hasa katika kilimo cha mimea cha Watonga wa Wilaya ya Binga ya Jimbo la Kaskazini la Matabeleland, na ufugaji wa kabila la Wakalanga la Wilaya ya Plumtree katika Jimbo la Kusini la Matabeleland. Utafiti ulilenga kubaini baadhi ya maarifa ya asili yaliyotumiwa na watu kuhimili maisha katika mazingira magumu ya hali ya hewa na ya maumbile ya nchi.

 Malengo mahususi katika Wilaya zote mbili za Binga na Plumtree yalikuwa: (i) kubaini athari za kijamii, kisiasa, kidini, kiuchumi na kimazingira za mifumo ya maarifa ya asili katika kilimo; (ii) kubaini na kuchambua mbinu za menejimenti (usimamizi) ya maliasili; na (iii) kutathmini thamani na upungufu wa mifumo ya maarifa ya asili katika kilimo.

 Mbinu za Utafiti

Taarifa zilikusanywa kupitia mapitio ya machapisho mbalimbali ya kitaaluma yanayohusiana na mada, mahojiano na wakulima, kutembelea maeneo ya kilimo, majadiliano katika vikundi na matumizi ya watafiti walioko vijijini. Watafiti walioko vijijini waliiandaa jumuiya kwa ajili ya utafiti wa uwandani na pia waliandaa majadiliano. Utafiti wa uwandani huko Kamaziya katika Wilaya ya Binga ulitembelea kaya 40; huko Plumtree takribani kaya 100 zilitembelewa.

 Matumizi ya Rasilimali

Katika Wilaya ya Binga, wanaume hudhibiti rasilimali za familia na kuona kwamba rasilimali hizo zinagawanywa na kutumiwa vema. Rasilimali hizi hujumuisha ardhi, maji, mazao ya mimea, mifugo, na nguvukazi ya familia. Ardhi hugawanywa kwa familia mpya na chifu wa eneo ambaye, kwa kushauriana na wazee wengine, hugawanya ardhi kwa ajili ya makazi na kilimo. Usimamizi wa ardhi na rasilimali zake katika Wilaya ya Binga hufanywa na Kamati za Maendeleo za Vijiji zilizoanzishwa na serikali miaka ya 1980.

 Wakazi wa Wilaya ya Plumtree hujishughulisha zaidi na kilimo cha kujikimu na ufugaji wa wanyama. Ingawa mbao ni nyingi, wakazi wa eneo hili huona kuwa rasilimali hizi hazitumiwi kwa ufanisi kuwa chanzo cha ajira na mapato. Mbao nyingi hutumika kama kuni na kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na nyua.

 Desturi za Mifumo ya Maarifa ya Asili

Mifumo ya Maarifa ya Asili imo katika maeneo yote mawili na bado inawahimilisha wanavijiji katika ukulima wa mazao - ikiwa ni pamoja na utayarishaji wa ardhi, uchaguaji wa nafaka, upandaji, uvunaji, na kadhalika uhifadhi wa nafaka na usimamizi wa mifugo.

 Desturi iliyozoeleka zaidi ya mifumo ya maarifa ya asili ya Wakalanga ilihusu maarifa yao ya asili ya nyasi na udongo unaofaa kutengwa kwa ajili ya malisho. Viongozi wa familia walikutana nyumbani kwa chifu kila majira ya kuchupua ili kujadili mipango ya malisho kwa majira hayo. Tarehe za kuanza na kumaliza kuchungia katika malisho maalum pia zilipangwa kisha wajumbe na wakuu wa vijiji walisimamia utekelezaji wa wanavijiji wa kanuni hizi.

 Jumuiya zote mbili za Binga na Plumtree walithamini mambo matatu kuhusiana na mifumo ya maarifa ya asili. Kwanza, maarifa ni nguvu. Watu walioishi Plumtree kwa miaka mingi walifahamu ruwaza za mvua na vipindi vya kupanda mazao ili kupata mavuno mazuri. Thamani ya pili ya mifumo ya maarifa ya asili ilihusu msingi wa maarifa unaowezesha ugawanyaji mzuri wa chakula na pia mgawano mwafaka wa kazi. Jambo la tatu muhimu mintarafu mifumo ya maarifa ya asili lilihusiana na upatikanaji wa hudumu wa rasilimali kwa ajili ya maisha endelevu.

 Hitimisho

Wakati wa utafiti wake wa uwandani, mwandishi wa makala hii aligundua jinsi jumuiya za wenyeji zinavyoithamini mifumo ya maarifa ya asili. Makabila yote mawili ya Watonga na Wakalanga wanathamini mifumo ya maarifa ya asili kama msingi wa maarifa na wa uzalishaji wa chakula na ugawanaji wa kazi kati ya jinsia na marika na pia kama sehemu ya uendelevu wa uhai wao. Mwandishi anapendekeza kwamba mifumo ya maarifa ya asili ijalize, badala ya kushindana na ile ya Magharibi, katika utekelezaji wa miradi. Funzo kwa mashirika ya kimaendeleo sharti liwe kuchunguza kwanza nini wenyeji wanajua na wanacho, na kisha kuziendeleza na kuziboresha teknolojia za asili.

 Katika Wilaya ya Plumtree, wananchi walionyesha kwamba ukame unaotokea mara kwa mara na kukosekana kwa nyasi na ardhi za malisho umefanya uchungaji wa mzunguko, ambao ni wa mapokeo, kuwa ngumu. Athari za Magharibi pia ziliitishia mifumo ya maarifa ya asili. Wilaya ya Binga ilionyesha kuwa mbinu za kulima za asili zimeachwa na badala yake zinatumika zile za Magharibi; mazao ya mapokeo yamebadilishwa na mazao ya biashara.

 Moja ya upungufu wa mifumo ya maarifa ya asili ni kukosekana kwa nyaraka inayohusu mifumo hiyo. Maarifa ya Waafrika juu ya mimea ya asili pamoja na majina yake yanapungua kwa kasi kubwa. Ubora wa mifumo ya maarifa ya asili ni finyu pia kutokana na maarifa haya kutokitwa kwa utafiti wa kisayansi. Kinachoelezwa zaidi ni kwamba ni mwiko kufanya mambo fulani. Mifumo ya maarifa ya asili pia ina hatari ya kutoweka kwa vile inategemea wale wanaohadhi maarifa hayo kuwa tayari kuwagawia wenzao. Aidha vijana wengi huyaona maarifa haya kuwa yamepitwa na wakati ikilinganishwa na maarifa ya utamaduni na desturi za Magharibi.

 Utafiti unapendekeza mambo yafuatayo:

 ·    Andaa programu imara za utambuzi wa mifumo ya maarifa ya asili na nafasi yake katika menejimenti (usimamizi) ya utumiaji wa rasilimali.

·     Tafiti, weka katika nyaraka na sambaza taarifa za kina kuhusu mifumo ya maarifa ya asili.

·    Kuza na hamishia mifumo ya maarifa ya asili kwenye maeneo yenye sifa bainifu zinazofanana. Kutembeleana baina ya vikundi vinavyoendesha miradi inayofanana ni njia mojawapo ya kutekeleza azima hii, kama zifanyavyo warsha juu ya masuala muhimu ya mifumo ya maarifa ya asili.

·    Toa machapisho juu ya mifumo ya maarifa ya asili, hasa katika lugha za kienyeji za jumuiya lengwa.

·    Patia mafunzo wafanyakazi wa mashirika ya maendeleo, hasa wale wanaofanya kazi moja kwa moja na jumuiya za asili.

·    Jenga uwezo wa wenyeji wa kutambua thamani ya mifumo ya maarifa ya asili na kuza mifumo hii kupitia: mikusanyiko ya kimapokeo ya jumuiya; mafunzo juu ya utafiti wa mifumo ya maarifa ya asili; uandaaji nyaraka na usambazaji wake; na msaada toka sekta rasmi wa kuziwezesha jumuiya za asili kuendeleza zenyewe mifumo ya maarifa ya asili.

 Makala hii iliandikwa na Harold Sibanda, Ofisa Mipango wa Umoja wa Vyama vya Vijiji kwa Maendeleo ya Bulawayo, Zimbabwe. Imerudiwa kuchapishwa kutoka Perspectives on Indigenous Knowledge Systems in Southern Africa na Jeri Larson, April 1998, Discussion Paper No.3, Environment Group, Africa Region, WB. Kwa maelezo zaidi wasiliana na Jeri Larson, Rm J8 - 120, World Bank, 1818 H Street, NW, Washington D.C 20433. Tel. No (202) 4734333.

E-mail: jlarson@worldbank.org

[Back to TOC]


Footer