THE WORLD BANK GROUP A World Free of Poverty
Home

[Back to TOC]

Matumizi ya Elimu ya Kurani katika Nchi za Afrika Magharibi

Ni stadi zipi halisi ambazo wanafunzi huzipata katika viwango mbalimbali vya elimu ya kurani huko Afrika Magharibi? Kuna matumizi gani ya kila siku ya elimu hiyo na mitandao gani hutumika katika kuikuza na kuitumia elimu hiyo? Elimu ya kurani katika aina zake mbalimbali kwa muda mrefu umekuwa mfumo sambamba wa elimu katika bara lote la Afrika – mfumo ambao umekuwepo kwa karne nyingi, lakini bado haufahamiki sana na wataalam wa mipango ya maendeleo na hivyo kwa nadra sana huzingatiwa katika sera na mikakati ya wataalam hao.

Uislamu una historia ndefu Afrika Magharibi na mifumo ya elimu ya kiislamu kwa hakika imekuwa ikitumika huko kwa muda mrefu zaidi kuliko ile ya Magharibi. Imani ya Kiislamu iliingia kwa mara ya kwanza huko Afrika ya Kaskazini kwenye karne ya 7. Ilipofikia karne ya 10, jumuiya za wafanyabiashara na wasomi wa Kiislamu zilikuwa tayari zinaishi kwenye vituo vya kibiashara vya Sahara ya Magharibi na Sahel. Ilipofikia karne ya 11 au ya 12, watawala wa falme kama vile za Takrur, Ghana ya Kale na Gao, tayari walikuwa wameshasilimu na kuwateua Waislamu wajuzi wa Kiarabu kuwa washauri wao.

Biashara ya kuvuka Jangwa la Sahara ilishamiri zama za kabla ya ukoloni na ikahusisha idadi kubwa zaidi ya bidhaa zilizobadilishwa kati ya Afrika na Ulaya kuanzia karne ya 11 hadi ya 16 – yaani hadi kabla ya kuwasili vyombo vya Ulaya kwenye Pwani ya Afrika Magharibi na kuanzishwa kwa biashara ya utumwa ya kuvuka Bahari ya Atlantiki na biashara ya pembe mraba baina ya Afrika, Ulaya na Dunia Mpya iliyokuwa matokeo ya biashara ya kuvuka Sahara. Awali msingi wa biashara ya kuvuka Sahara ulikuwa mitandao ya miji iliyoanzishwa kwenye njia za biashara na wafanyabiashara kutoka Afrika Kaskazini, ambao hatimaye walilowea na/au nafasi yao ikachukuliwa na wenyeji. Kodi iliyotokana na biashara hii ilichangia sana kwenye mapato yaliyohitajika kwa ajili ya ujenzi wa nchi/dola.

Muundo wa Mfumo wa Mafunzo ya Kurani

Mfumo wa mafunzo ya Kiislamu katika Afrika Magharibi nzima unajumuisha ngazi kadhaa ingawa haziko waziwazi mno kama zile za mfumo wa Ulaya Magharibi. Zaidi ya hapo, kwa  sasa unajumuisha muundo wa kimapokeo (mfululizo asilia wa mafunzo ya Kurani), shule rasmi au ya “kisasa” (shule za mchanganyiko wa Kifaransa na Kiarabu, pengine huitwa ‘madrasa’), na vidato vya kati ambavyo hujulikana kama “elimu ya kurani iliyoboreshwa”. Ngazi ya chini kabisa ya muundo wa kimapokeo ni ‘maktab’ au shule za Kurani za ngazi ya msingi ambako watoto wa miaka 3 hadi 10 huanza kujifunza Kurani na majukumu ya msingi ya maisha ya Kiislamu. Ngazi inayofuata ni ya ‘madris’ au shule za sekondari ambako wale waliomudu kukariri na kunukuu sehemu kubwa ya Kurani huendelea kusoma kile kinachojulikana kama “sayansi ya Kiislamu” (‘ilm’), ikiwa ni pamoja na maandiko muhimu ya dini na taaluma nyinginezo. Wanafunzi wachache huendelea mbele kwa mafunzo ya juu zaidi chini ya maimamu na mamurabiti mashuhuri au katika vyuo vikuu vya Kiislamu vya Afrika Kaskazini na nchi nyingine za Kiislamu.

Walau katika ngazi ya msingi – inayowakilishwa na shule za kurani za maeneoni – mafunzo ya Kiislamu yameenea kote Afrika Magharibi. Huko Niger peke yake kulikadiriwa kuwepo na takribani shule 40,000 za kurani mwaka 1990. Aina hii ya elimu ni maarifa muhimu mbadala (wa elimu rasmi na ya Magharibi) na aghalabu huchanganyika na pengine kushindana na elimu rasmi, ingawa katika nchi nyingi za Afrika asasi za msingi za mfumo wa Kiislamu yaani ‘maktab’ – hazijachukuliwa kama shule kabisa. Pamoja na hayo, wanafunzi, walimu na waumini wa Kurani kote Afrika Magharibi wanatambua fika historia ndefu ya imani yao na wasomi na walimu wake mashuhuri, baadhi yao wakiwa na madaraka makubwa ya kisiasa na kiuchumi, hasa katika eneo la Sahel. Mathalani, wale wanaojishughulisha kwa miaka mingi na biashara ya mazao huko Niger, Mali na Senegal wameimarisha mitandao ya biashara ya mitaji mikubwa hasa katika sekta ya mashamba na viwanda nchini mwao, na pia nchi za nje. Mambo yote haya yanazidi kuwa kivutio kwa elimu mbalimbali za Kurani kama mfumo mbadala wa kufikia usitawi wa kiuchumi au kisiasa. Kwa ufupi, kuna mwingiliano mkubwa wa utamaduni baina ya mataifa.

Ubora unaotofautiana, uenea mkubwa

Licha ya hali hii ya kufanana kimsingi kwa utamaduni na mafunzo ya kidini, hali halisi na ubora wa mafunzo katika shule za Kurani na mfumo wa Kiislamu kwa ujumla hutofautiana sana kutoka sehemu moja hadi nyingine. Katika sehemu zenye waumini wengi wa Kiislamu, idadi kubwa zaidi ya watoto huhudhuria shule za Kurani. Kimsingi hawa hujifunza kupitia mbinu ya kukariri msahafu. Wengi wa wanafunzi ni wavulana, lakini aghalabu kwa uwiano usiozidi 3/2 au 2/1 katika ngazi za mwanzoni. Katika sehemu chache kama vile Futa Jalon huko Guinea, idadi ya wavulana na wasichana kwa jumla ni kama imelingana.

“Kina” cha mafunzo ya Kiislamu katika maeneo haya ni tofauti sana, lakini kwa kawaida idadi ya kutosha ya wanafunzi wavulana wanaendelea baada ya masomo ya awali ya Kurani hufikia hadi ngazi fulani za elimu ya juu. Kwa kuwa uelewa wa Kiarabu cha kisasa ama cha kimapokeo nje ya msahafu wenyewe ni mdogo sana, (isipokuwa kwa wale waliosomea kwenye nchi zinazozungumza Kiarabu), kiwango cha juu kabisa cha uelewa – yaani, uwezo wa kusoma na kuandika, kuweka rekodi na maandiko mbalimbali kwa ujumla – hupatikana aghalabu kwenye nyanda za juu za Guinea, eneo la Sine Saloum la Senegal, na maeneo ya wazungumzaji Kihausa ya Niger, ambako kuna mfumo wa unukuzi ulioendelea wa lugha za Kiafrika unaotumia herufi za Kiarabu (ambazo huitwa ‘ajami’ katika Kihausa na Kifulani). Nchini Guinea, asilimia 93 kati ya wahitimu wanaume 77 wa Kurani waliohojiwa walidai kuweza kusoma na kuandika katika ‘ajami’. Nchini Senegal, kati ya asilimia 25 na 75 ya wanaume waliohojiwa vijijini, na kati ya asilimia 10 na 25 ya wanawake, walidai kuwa na kiwango sawa cha uelewa. Kwa kila hali, kiwango hiki cha uelewa kwa jinsia zote mbili kilizidi uelewa wa Kifaransa kwa jumuiya hizi ambazo kimsingi ni za vijijini.

Kwa upande mwingine, asilimia 26 tu ya sampuli ya Guinea ya wanafunzi wa zamani wa Kurani walijichukulia wanajua “kuhesabu” ikilinganishwa na asilimia 93 waliojichukulia kuwa wanaweza kuandika katika ‘ajami’. Hata hivyo, wengi wa mamurabiti na maimamu yaelekea walijifunza kuhesabu kwa namna moja au nyingine, jambo linaloelezea sababu za kuwakuta wengi wao wakishughulikia masuala ya mahesabu ya fedha katika jumuiya nyingi.

Wakati ufundi stadi hauzingatiwi sana katika mafunzo ya Kurani, wengi wa wanafunzi wanaoendelea na masomo baada ya yale ya msingi hujikuta wakifanya uanagenzi chini ya mamurabiti ama mafundistadi au wafanyabiashara, ili kupata fedha za kujikimu na kugharamia masomo. Elimu ya Kurani huelekea kuwa na kipengee cha mafunzo ya mazoezi katika jumuiya, ingawa huchukua sura ya mafunzo ya kiufundi stadi wakati mwingine; na wanafunzi wa Kurani hujazwa na dhana kwamba watahitajika kujitegemea wenyewe au kutafuta wafadhili mwafaka watakapofikia umri fulani. Hii ndiyo iliyompelekea mtafiti mmoja wa Kisenegal kusema “shule za Kurani hufundisha wabunifu wa ajira, ilihali mfumo wa elimu rasmi hufundisha watafutaji wa ajira”.

Matumizi ya Mafunzo ya Kurani

Matumizi makuu binafsi ya mafunzo ya Kurani ni kuandika na kuwasiliana, na ajira maarufu kabisa kwa wahitimu waliobobea wa Kurani ni kuwa mamurabiti au maimamu , kwa vile kuna mahitaji makubwa ya walimu na wahudumu wa kidini; kutokana na kuenea kwa haraka kwa Uislamu huko Afrika Magharibi kwenye miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo zaidi ya robo ya wahojiwa wa Guinea walisema kuwa ajira katika sekta ya huduma za umma ni matokeo ya mafunzo yao. Dai hili hujitokeza pia katika eneo zima la Afrika Magharibi.

Hata hivyo, yapo pia matumizi ya pamoja kwa kiwango cha kutosha. Maadili, sheria na mamlaka ya Kiislamu yametumika sana kama msingi wa uongozi wa kimapokeo kwa karne nyingi katika eneo lote la Sahel. Kusema kweli, msamiati mwingi katika lugha kuu za Kisahel sio tu unahusu dini, bali pia sheria, utawala, itifaki na elimu ya juu na hali kadhalika umetokana moja kwa moja na Kiarabu ama umekopa manenno mengi toka lugha hiyo.

Hitimisho:Njia mbadala za kupatia elimu

Kutokana na hali iliyoelezwa hapo juu, mafunzo ya msingi ya Kiislamu – yale yanayotolewa katika shule za Kurani – yana matumizi na athari za aina tatu kuu katika Afrika Magharibi hivi leo:

·         Hutoa msingi wa teknolojia ya kuandika – na kwa kiasi fulani, ya kuhesabu – kwa idadi ya kutosha ya wananchi, wanaume na wanawake, ambao, vinginevyo wengi wao wangekuwa na elimu ndogo kabisa ama wasingekuwa na elimu.. Wale wanaojiendeleza na kuwa mahiri katika kusoma, kuandika na kuhesabu (hasa katika lugha za Kiafrika, kwa vile umahiri katika Kiarabu ni ngumu zaidi) kwa kawaida huwa ni wachache, ingawa katika baadhi ya maeneo idadi yao ni kubwa kidogo. Zaidi ya hapo, kufahamu maandiko ya Kiarabu sasa hivi huchukuliwa na watu wengi vijijini na mijini kuwa ni hali ya “kutoelimika” kwa mtazamo wa kimagharibi.

·         Huchukuliwa pia kuwa ni mafunzo kwa ajili ya uongozi, kwa vile mafunzo halisi ya Kiislamu kwa kawaida huchukuliwa kuwa ni kionyeshi cha uadilifu, uaminifu na nidhamu na hivyo kuwa sifa muhimu ya mtu kupatiwa nafasi ya madaraka.

·         Zaidi ya hapo, mafunzo hayo daima yamekuwa – na kutokana na chuki ya hivi karibuni dhidi yya elimu rasmi, yamezidi kuwa – daraja la kupatia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kutokana na uhusiano wa karibu kati ya mitandao ya Kiislamu na ile ya biashara ya kimapokeo katika eneo lote. Wahitimu wa shule za Kurani wana nafasi kubwa zaidi ya kupata ajira au uanagenzi kutoka kwa wafanyabiashara wa kimapokeo na katika sekta isiyo rasmi ya uchumi.

*Msingi wa makala hii ni utafiti uliofanywa na watafiti wa Senegal kwa msaada na ushauri wa kiufundi wa Profesa Peter Easton wa Chuo Kikuu cha Jimbo la Florida, wakishirikiana na baadhi ya jumuiya za Kiafrika. Utafiti ulifadhiliwa na Club du Sahel?OECD, CILSS na ADEA.

 

[Back to TOC]


Footer