|
TIBA
YA KIENYEJI KWA WATOTO WALIOATHIRIWA NA VITA
KATIKA AFRIKA (Edward C. Green, Ph.D na Alcinda Honwana, Ph.D) Watoto katika nchi za Afrika na kwingineko zilizomo katika vita aghalabu huathirika moja kwa moja au vinginevyo na vurugu ya vita hivyo, au huwa mashahidi wa mateso mbalimbali yanayoambatana na vita hivyo. Watoto wadogo wenye umri wa miaka saba hadi nane huandikishwa kwa nguvu jeshini kama askari watoto ama wapagazi katika nchi kadhaa za Afrika. Wasichana pia wavulana mara nyingi kuteseka, wengine wakilazimishwa kutoa huduma za kimapenzi na nyinginezo wakiwa na umri mdogo kabisa. Katika migogoro ambamo vitisho kwa raia zimekuwa mbinu za kawaida za kupatia madaraka ya kisiasa na kijeshi, wanawake na watoto hulengwa kwa makusudi kupatiwa mateso na kisha kuuawa. Kwa ujumla, ulinwenguni kote wapo takribani watoto milioni moja waliotengwa na wazazi wao kutokana na vita, na kuna maelfu mengi ya watoto waliopata kihoro kwa sababu ya vita. Watoto waathirika wa namna hii aghalabu huonyesha dalili kadhaa ikiwa ni pamoja na: kukwepa au kuwa wazito katika kufanya mambo, kama njia ya kukwepa kukumbuka mambo yaliyowaletea kihoro siku za nyuma; kurukwa na usingizi, kushindwa kumakinikia mambo, kumbukizi ya mambo ya zamani kupitia majinamizi au makumbusho mengine ya ghafla; uchovu, kuchanganyikiwa, hofu, tabia ya ukandamizaji, kujitenga kijamii, na kutokuwa na matumaini ya baadaye na kujilinda kupita kiasi pamoja na kushughulikia kwa nguvu mno mishituko mbalimbali. Katika miaka ya hivi karibuni, UNICEF, USAID, na mashirika mengine ya binafsi ya kujitolea kama vile Mfuko wa Kusaidia Watoto na Mfuko wa Watoto wa Kikristo yameandaa programu mbalimbali za kisaikolojia ili kuwasaidia watoto walioathiriwa na vita. Hata hivyo, mbinu za kuwatibu watoto walioathiriwa na vita bado zimo katika hatua za awali za maendeleo. Bado haijaeleweka ni kwa kiwango gani mbinu za nchi za magharibi za kutibu waathiriwa wa vita zilizobuniwa awali kuwatibu maveterani wa Marekani wa vita vya Vietnam zitafaa kwa watoto wa Afrika na nchi nyingine zinazoendelea. Moja ya mambo yanayotatiza kuhusu magonjwa yatokanayo na vita ni dhana yenyewe ya ugonjwa baada ya athari za kihoro. Katika miktadha hii ni tatizo kuzungumzia kihoro kama jambo lililotukia nyuma, kama mtu anafahamu dhana ya vurugu kuwa pana zaidi ya kukabiliana moja kwa moja na mazingira ya kivita (mashambulio ya kijeshi, mabomu ya ardhini, n.k.), na kujumuisha nyanja nyingine kama vile umasikini, njaa, uhamisho na mambo mengine kama haya. Jambo jingine kuhusiana na magonjwa yatokanayo na vita ni mbinu za tiba zinazomhusu mgonjwa mahususi. Mbinu hizo aghalabu hazijali imani za kijadi katika dhima za mizimu katika kusababisha na kutibu mateso. Pia mbinu hizo zinadhoofisha ushiriki wa familia na jumuiya kaitka harakati za kutoa tiba. Wakati wa programu za awali za kisaikolojia na kijamii kwa ajili ya watoto walioathiriwa na vita nchini Msumbiji na Angola, viongozi wa jumuiya, waganga wa kienyeji na familia walionyesha ujuzi mkubwa wa kutibu “madhara ya kijamii” ya watoto na watu wazima walioathiriwa na vita. Madhara haya kwa kweli hutibika na waganga wa kienyeji wakitumia uelewa wa asili wa namna vita inavyoathiri mawazo na tabia za watu, na imani ya jinsi nguvu za mizimu zinavyosaidia katika harakati za tiba. Wakati wa utekelezaji wa programu hizi, watu hawakuonyesha kuhitaji msaada katika kukabili matatizo mahususi ya watoto ya kiakili na kitabia. Walichohitaji, kama walivyosema wao wenyewe, ilikuwa msaada katika kuwatafuta wanafamilia waliopotea na katika uanzishaji wa shule, shule za chekechea, kutafuta nafasi za ajira kwa ajili ya vijana, na kuboresha mazingira ya kijamii ya kufanyia kazi za uzalishaji mali. Kuna ushahidi kutoka Afrika nzima kwamba magonjwa ya akili au ukichaa ni miongoni mwa mambo yasiyohitaji sana msaada wa tiba ya kisassa au ya kimagharibi. Kwa kwaida Waafrika hutumia tiba ya kienyeji kwa magonjwa ya akili. Utafiti wa kimajaribio wa ufanisi wa tiba za magharibi za magonjwa ya akili unaoneysha kwamba tiba zote hizo humsaidia mgonjwa kwa kiasi fulani na zote kuwa na ufanisi zaidi zinapoambatanishwa na hali halisi ya kijamii na kiutamaduni. Hii inaonyesha kwamba kama matabibu, waganga wa kienyeji wa Kiafrika wanafaa kama walivyo wataalam wa kisasa wa tiba, hasa wale wanaoamini katika utamaduni wa Kiafrika. Utafiti wa kianthropolojia uliofanyika nchini Msumbiji na Angola unaonyesha kuwa kihoro cha kisaikolojia kinachohusiana na vita kimefungamanishwa moja kwa moja na nguvu na hasira za mizimu ya wafu. Kutowezekana kutimiza kikamilifu desturi na mila za mazishi wakati wa vita huifanya mizimu hii ya wafu kukasirika na hivyo kuleta madharaa kwa waliosababisha mauaji na kwa wapita njia. Uchafu wa kijamii waweza kujitokeza kutokana na kukabiliana na kifo na umwagaji damu. Watu waliokuwa vitani, walioua ama walioshuhudia mauaji kuchukuliwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuchafua mwili wa kijamii. Hivyo matambiko ya kuwatakasa ni muhimu yafanyike ili kuwarejesha tena watu wa namna hiyo katika jumuiya. Mwaka 1994, wakati wa mradi wa kwanza nchini Angola ulioandaliwa mahususi kuwasaidia watoto wenye kihoro kutokana na vita, ilibainika kuwa watoto tayari walikuwa wakisaidika na tiba asilia ya kisaikolojia, iliyokuwa ikitolewa na waganga wa kienyeji kupitia matambiko ya utakasaji. Huduma hii ilitolewa kwa waliokuwa wapiganaji na watoto ambao ama walishiriki katika vita ama walishuhudia umwagaji wa damu. Mradi wa awali wa Watoto na Vita nchini Msumbiji ulibaini matibabu kama haya kwa watoto. Katika nchi zote hizi mbili, matibabu haya yalionekana kufaa walau kwa muda mfupi. Tiba ya kienyeji kwa watoto walioathiriwa na vita nchini Angola na Msumbiji yaelekea kimsingi kujumuisha matambiko ya utakaso, yaliyohudhuriwa na wanafamilia na jumuiya kwa ujumla, ambapo mtoto alitakaswa “uchafu” wa vita na kifo, na pia wa dhambi, hatia, na kisasi cha mizimu cha watu waliouawa na askari mtoto. Sherehe hizi za matambiko zimejaa ishara zilizo mahususi kwa kabila husika, lakini zenye mada linganifu kwa takriban makabila yote. Siku aliyofika ndugu zake walimpeleka kwenye ndumba (nyumba ya mizimu). Hapo alikabidhiwa kwa mizimu mababu ya familia yake. Babu ya kijana alizungumza na mizimu akiijulisha kuwa mjukuu wake karejea na anaishukuru mizimu kwa ulinzi wao kwani mjukuu amerudi akiwa hai(…). Siku chache baadaye mtu mwenye uwezo wa kuwasiliana na mizimu alikaribishwa na familia ili kuwasaidia kuendesha matambiko ya kumtakasa kijana wao. Mtu huyo mwenye uwezo wa kuwasiliana na mizimu alimchukua kijana hadi msituni, na huko kibanda kidogo kilichofunikwa na nyasi kavu kilijengwa. Kijana, akiwa amevaa nguo chafu alizotokanazo kwenye kambi ya RENAMO, aliingia kibandani na kuvua nguo yeye mwenyewe. Kisha kibanda kilichomwa moto, na ndugu mtu nzima alimsaidia kijana kutoka nje ya kibanda hicho. Kibanda, nguo na kila kitu kingine alicholeta kijana kutoka kambini vilipaswa kuteketezwa kwenye eneo la matambiko. Baada ya hayo, kijana alivuta moshi wa dawa fulani za majani, na kuoga kwa maji yaliyotiwa dawa. (Notisi za uwandani, Msumbiji) Tambiko hili la uponyaji linaweka pamoja mfululizo wa maana za kiishara zinazolenga kukata uhusiano wa mtoto na zama za kale (za wakati wa vita). Wakati tiba ya kisaikolojia ya kisasa inasisitiza kuyatoa nje mateso kwa kutumia maneno, hapa kwa kupitia maana za kiishara kama za kale zinafungwa nje. Hii inaonyeshwa kwa kuchoma kibanda na nguo na kwa utakaso wa mwili. Kuzungumzia au kukumbushia zamani si lazima kuonekane kama kitangulizi cha tiba au kupunguza maumivu. Kwa hakika, hali hii huaminika kuwa ndiyo inayofungua fursa kwa nguvu za giza kuingilia harakati za tiba. Hii imedhihirika pia kwenye mfano ufuatao kutoka Uige (Angola). Wakati mtoto au kijana arejeapo nyumbani, hulazimika kusubiri nje ya kijiji. Mwanamke mzee kuliko wanawake wote kijijini humwagia kijana unga wa mahindi na kumpaka mwili mzima mafuta ya kuku. Ni baada tu ya kutimiza tambiko hili ndipo kijana anapoweza kuingia kijijini. Baada ya tambiko kijana kuruhusiwa kuisalimu familia yake kijijini. Baada ya maamkizi hayo, ni lazima kijana achinje kuku, ambaye hupikwa na kuliwa na wanafamilia. Kwa siku nane za kwanza baada ya kurejea nyumbani, kijana haruhusiwi kulala kwenye kitanda chake, bali hulala chini kwenye mkeka wa matete. Katika kipindi hiki, kijana kupelekwa mtoni na maji humwagiwa kwenye kichwa chake na hupatiwa muhogo ale. Anapoondoka kwenye eneo la tambiko, hapaswi kabisa kugeuka nyuma. Mfumo huu unasisitiza kutokuwepo kwa maingiliano na familia na marafiki kabla ya tambiko la utakaso. Mtoto kuzuiliwa nje ya kijiji hadi tambiko lifanyike, na hawezi kuwasabahi watu na kulala kwenye kitanda chake hadi taratibu za matambiko zinapokamilika. Kama ilivyoelezwa hapo juu, ingawa watoto wanaweza kuulizwa juu ya uzoefu wao wa vita kama sehemu ya tiba, jambo hilo sio sharti la msingi la tiba. Sherehe hulenga kumtakasa mtoto kiishara na kumfanya asahau kabisa uzoefu wake wa vita. (Zingatia ishara za kukatazwa kutazama nyuma kwenye mfano wa Uige). Miko ya chakula na makatazo mengine ya matambiko hutumika. Huko Uige, kwa mfano, samaki na ndege hukatazwa kwa mtu aliyetakaswa kwa mwezi 1 hadi 2, na bada ya hapo mtu huyo lazima aruhusiwe kula vyakula hivyo na mganga wa kienyeji aliyeendesha tambiko la utakaso. Tambiko la “Okupiolissa” kutoka Huila nchini Angola linaonyesha wazi ushiriki wa kiwango cha juu wa jumuiya kwenye matambiko haya, na kusisitiza wazo la kutakasa “uchafu”. Kwa kawaida jumuiya na wanafamilia husisimka na kufurahia wakati kijana anaporejea nyumbani. Wanawake hujiandaa akwa sherehe za maamkizi (…) Kiasi fulani cha unga unaotumika kupakwa kwenye mapaji ya uso ya wanawake hutupiwa mtoto na mwanamke mkongwe anayeheshimika kijijini hutupa kibuyu kilichojaa majivu miguuni mwa mtoto. Wakati huohuo, kijana humwagiwa maji safi kama njia ya kumtakasa (…) Wanawake wa kijijini hucheza wakimzunguka mtoto huku wakitoa ishara kwa kutumia mikono ya kuifukuza mizimu isiyotakiwa au athari zisizohitajika (…) Kila mmoja wao humgusa mtoto kwa mikono yote miwili kutoka kichwani hadi miguuni ili kutakasa uchafu. Ngoma hii hujulikana kama: Ululando-w-w-w. Tambiko linapokamilika, mtoto kupelekwa kijijini kwake na wanakijiji husherekea kurejea kwake. Tafrija kufanyika kayani mwake ambako vinywaji vya kienyeji tu hutumika (…) Mtoto lazima akabidhiwe rasmi kwa machifu na wazazi wake (…). Mtoto hukaa pembeni mwa machifu, akinywa na kuongea nao, na tendo hili hyonyesha mabadiliko ya hadhi yake kijijini. Matambiko haya ya utakaso yanayohusisha askari watoto yanafanana na kile wananthropolojia wanachokiita kaida za mabadiliko. Yaani, mtoto hupitishwa katika mabadiliko ya kiishara ya hadhi kutoka mtu aliyeishi kwa kuvunja taratibu njema za maisha (yaani, kuua, vita) na kuwa mtu ambaye sasa anapaswa kuishi kwa amani na uadilifu, kulignana na kaida za jamii yake. Katika mfano uliotolewa juu kutoka Huila, mtoto aliyetakaswa huchukua hadhi mpya inayomruhusu kuketi pembeni mwa machifu na kuongea nao. Hadi mabadiliko yanapokamilika (kupitia matambiko), mtoto kuchukuliwa kuwa katika hali ya hatari na yenye utata. Kwa sababu hii, mtoto hawezi kurejea kwenye familia au kibanda chake, au kulala katika kitanda chake, au pengine hata kuingia kwenye kijiji chake, hadi matambiko yamekamilika. Dalili husianifu na magonjwa ya kihoro kinachotokana na athari za vita yameripotiwa kutoweka muda mfupi baada ya sherehe hizi, na baada ya hapo familia, wanganga wa kienyeji na machifu huelekeza nguvu zao kaitka kusaidia kuleta mahusiano ya kudumu na ya kuaminiana baina ya mtoto mwenye mateso na wanafamilia yake na kadhalika watu wazima wenye tabia njema. Matambiko haya vilevile yamelenga kuanzisha upya upatanifu wa mizimu, hasa ule baina ya mtoto na mizimu ya mababu zake. Uanzishaji upya wa mahusiano ya kawaida na shughuli na watoto wengine waweza usiwe sehemu –au sehemu kuu -ya matambiko haya ya kienyeji ya tiba. Lakini, waganga, wazee wa vijiji, walimu na watunzaji wengine wa watoto wanalielewa hili fika wanapoulizwa kwenye semina za mafunzo zinazofadhiliwa na mradi, nchini Angola na Msumbuji. Tiba kwa kutumia michezo, michoro, drama, ngoma na masimulizi ya hadithi ni baadhi ya mbinu zinazofundishwa kwenye semina hizi. Hapana shaka kwamba matambiko haya yanasaidia kujenga mshikamano wa familia, na kukabili matatizo ya kisaikolojia, kijamii na kimhemko ya watoto. Ukweli, hata hivyo, ni kwamba watoto hawa hurejea kwenye vijiji fukara vinavyopambana kupata mahitaji yao ya maisha, na idadi kubwa ya vijiji hivyo havina shule, hospitali, vyuo vya ufundi stadi au nafasi za ajira – fursa ambazo zingewezesha kuwa na maisha mazuri zaidi ya baadaye. Hivyo ingawa matambiko haya ni muhimu, yanahitaji kujalizwa na programu za maendeleo za jumuiya ili kudumisha mafanikio yaliyopatikana kwenye nyanja za kisaikolojia, kijamii na kimhemko, na ambayo hayawezi kutengwa na maendeleo katika sekta nyinginezo. Kwa hiyo mkabala wa mashirika ya wafadhili, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na mashirika mengine yanayotoa misaada ya kibinadamu kwa watoto walioathiriwa na vita hauna budi kuzingatia uelewa wa wenyeji wa mateso ya vita na mikakati yao ya kukabiliana na mateso hayo. Mashirika hayo yanapaswa kukuza mazingira imara, salama na yanayozingatia utamaduni ambamo watoto wanaweza kupata umilisi na hakika katika ulimwengu unaotabirika zaidi kwa kutilia shime ari ya kujitegemea kupitia miradi ya maendeleo ya kutumainiwa ya jumuiya, familia zao, ama familia mwafaka za walezi pale inapolazimika. Mradi wa Mfuko wa Watoto wa Kikristo nchini Angola unajaribu kuimarisha taratibu zilizopo za tiba ya kienyeji, huku ukizijaliza kwa tiba za kisaikolojia na kijamii kama zile zilizojadiliwa hivi punde. Tathmini za mradi huu na mradi wa awali wa “Watoto na Vita” nchini Msumbuji zimeonyesha kwamba ushirikiano wa namna hii usio rasmi kati ya waganga wa kienyeji na matambiko yao, na programu zinazosaidiwa na wafadhili, zikisisitiza juu ya familia na ujirekebishaji wa kijamii wa mtoto, unaweza kutoa mfano wa jinsi mikabala ya kienyeji na ya Kimagharibi - kisayansi inavyoweza kuchanganywa pamoja kutoa manufaa makubwa zaidi kwa watoto wenye dhiki. Zaidi ya hayo mfano huu wa ushirikiano na kuchangia majukumu unathibitisha tiba na imani za kienyeji, ambazo huwatia nguvu na hamasa wenyeji ambao hatimaye wanahitaji kukuza masuluhisho endelevu na yanayokubalika kiutamaduni ya kutatua matatizo yao na, hivyo, kusitawisha maendeleo yao wao wenyewe. Kwa Taarifa Zaidi Soma: Dawes, A. and A. Honwana, 1996, “Children, Culture and Mental Health: Interventions in Conditions of War”. Rebuilding Hope: Congress on Children, War and Persecution. Maputo, Mozambique, December 1996. Green, Edward C, and Mike Wessels, 1997 “Evaluation of the Province-Based War Trauma Team Project in Angola” (a project of the Christian Children’s Fund, Richmond, Va). Washington, D.C., April 1997; USAID (Displaced Children and Orphan’s Fund) and TvT Associates Arlington, Va, April 1997. Green, Edward C., Jan Williamson, Paula Nimpuno-Parente, Evaluation of Children and War Program, Washington D.C.: Academy for Educational Development/PRITECH evaluation, July 1992. Honwana, A. 1994. “Traditional Religious Instituitons and the Social Reintegration of Vulnerable Groups”. Research Report for the Swiss Cooperation for Development in Mozambique. Honwana, A. 1997 “Sealing the Past, Facing the Future: Trauma Healing in Mozambique”. Accord no. 3, Special edition on the Mozambican peace process, London: Coalition Resources. Honwana, A., 1997. Healing for Peace: Traditional Healers and Post-war Reconstruction in Southern Mozambique”. Peace & Conflict: The Journal of Peace Psychology. Vol. 3 no 3, New Jersey: Lawrence Earlaum Associates. Honwana, A. 1998 “Okusiakala Ondalo Yokalye (Let us Light a New Fire): Local Knowledge in the Post-War Healing and Reintegration of War-Affected Children in Angola” Consultancy Report for Christian Chidlrens Fund. Honwana A. 1998 (forthcoming) “Negotiating Post-War Indentities: Child Soldiers in Mozambique and Angola”. In G. Bond & N. Gibson (eds) Contested Terrainsand Constructed Categories: Contemporary Africa in Focus. New York: Westview Press. Honwana, A. & Pannizo, E. 1995 “Evaluation of the Children and War Project in Mozambique”. Research Report for Save the Children US and USAID. Kwa ripoti za USAID tazama Llyod Feinberg , feinberg@usaid.gov Pia kutoka Archive of Applied Anthropology Materials (J. van Willigen, ed). University of Kentucky: BITNETANTIOI@ukcc or (606257-6920 Waandishi Waandishi wangependa kushukuru Mfuko wa Watoto wa Kikristo, Saidia Watoto (Marekani), Mradi wa Watoto na Vita na Mfuko wa Watoto Wakimbizi na Mayatima, USAID, kwa kutumia taarifa kutoka kwenye programu zao. Vilevile tunamshukuru Mike Wessels kwa maoni yake. Edward C. Green anapatikana: egreendc@aol.com Alcinda Honwana anapatikana” honwana@beattie.uct.ac.za |