|
MIFUMO
YA MAARIFA YA ASILI KATIKA AFRIKA KUSINI MWA SAHARA:KWA MUHTASARI Watu wa vijijini barani Afrika daima wamehifadhi nguvu fulani za kutisha zinazolinda taasisi za asili na mifumo ya maarifa ya asili na kwa kufanya hivyo wameweza kudumisha kiwango fulani cha kujitegemea. Nguvu hizi zimekitwa kwa uwezo wa kuyakataa mambo ambayo hawana sauti nayo. Ripoti za hivi karibuni kutoka kwa mashirika ya wahisani zinazoelezea kushindwa kwa miradi ya kupunguza viwango vya umasikini barani Afrika kwa kipindi cha miaka ishirini iliyopita, zinathibitisha mtazamo huu. Miongo hii ya mipango iliyoshindwa kutekelezeka haikutokea kwa sababu wafanyakazi wa mashirika ya uhisani hawakuwa na moyo wa kufanya kazi, wala si kwa vile jumuiya za Kiafrika hazikupenda maendeleo. Miradi haikutekelezeka kwa sababu sauti za wanavijiji - ushirika na udhibiti wao ulichukuliwa kuwa ni sehemu ya lengo la maendeleo, na sio njia (mchakato) yenyewe ya maendeleo. Nguvu za watu wa vijijini za kukataa miradi ya maendeleo yenye mtazamo huu kwao, na inayowajumuisha kama "wafaidikaji" tu, lakini sio "watendaji" bila shaka hazijapanua msingi wao wa viingiziamali; na sasa uharibifu wa mazingira na kuzorota kwa uchumi kumeudhoofisha zaidi msingi huo. Pamoja na matatizo yote haya, watu wengi Afrika kote wanaamini kwa dhati kwamba maendeleo chanya mapya yanaweza kutokea, lakini iwapo tu watu wenyewe watadhibiti viingiziamali, uchumi na utamaduni. Hata hivyo, uwezo huu wa wananchi kudhibiti mambo yao, hutokea tu pale wananchi wanaporuhusiwa kufanya kazi ndani ya, kupanua na kubadili taasisi zao na mifumo yao ya maarifa. Hivyo fursa za kuleta pamoja mifumo ya maarifa ya asili na uhifadhi wa maliasili ni nyingi- lakini hatari pia ni nyingi. Fursa ni uwezekano wa kuanzisha miradi ya usitawishaji wa maliasili inayoendana vema na taasisi na mifumo iliyopo na hivyo kuwa endelevu. Hatari yake ni kwamba mazao yanayotokana na maarifa ya asili - ubainishaji wa mipango, au mbinu za upangaji mipango, kwa mfano - huweza kubainishwa bila kujali vipengee vyake vingine vya kanuni na dhima-ambavyo pia ni muhimu sana kwa vile aghalabu havionekani kwa mtu wa nje. Muunganiko wa namna hii unapotokea, umiliki ambao ni muhimu kwa uendelevu na kujitegemea huanza kudhoofika; na wananchi hujikuta wamepokonywa zaidi urithi wao wa kujitegemea. Lengo la makala hii ni kuelezea baadhi ya fursa ili ziweze kuendelezwa kwa ufanisi zaidi. Ili kutimiza lengo hili, masuala kadhaa yanajadiliwa kwa kifupi hapa chini ambayo yanahusiana na hatari na fursa hizo. Kuelezea
Tumefika Wapi Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 iliyopita, jumuiya ya maendeleo ya kimataifa ilichukulia kwamba mtindo wa maendeleo wa kuingiza pembejeo na kuzalisha mazao ndio ulikuwa muhimu zaidi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi. Hata hivyo, kushindwa kwa programu na taasisi hizi kupata uendelevu na ufanisi, ambayo ni matokeo muhimu ya mtindo wa uchumi wa "pembejeo - mazao", hatimaye kumesababisha mkabala huu wa uchumi kutiliwa mashaka. Utambuzi wa hali hii umesababisha kuiacha mifumo ya uchumi inayoanzia juu kwenda chini na kuzingatia zaidi mifumo shirikishi inayohusu nyanja zote za maendeleo ya wananchi. Nguvu ya mkabala huu mpya ni kwamba sio tu unatoa ufumbuzi mpya wa matatizo; bali pia unatoa ufumbuzi mpya wa kutambua matatizo. Jambo linaloweza kutuonyesha tumefika wapi katika kuzingatia mitazamo hii mipya ni kuangalia mabadiliko yaliyokwisha tokea katika kufasili matatizo yaliyopo. Hapa "hoja ya uendelevu" imetimiza yale yaliyoshindikana kutimizwa na dhana za "usawa" na "mahitaji ya msingi ya binadamu". Yaani kuonyesha kuwa maendeleo yanayowategemea na kuwashirikisha watu sio tu hupendelewa kwa vile yanazingatia haki, bali pia yanahitajika kutokana na ufanisi wake. Hata hivyo, utambuzi huu unaolingana wa matatizo, haumaanishi kuwa utatuzi wa matatizo hayo umelingana pia. Kwa hakika hakuna ulinganifu wa namna hiyo. Hatari hapa ni ya aina mbili. Kwanza, wale ambao wamekuwa wakiunga mkono mabadiliko haya kwa miongo mingi wanaweza wakaendelea kudhani kwamba hapakuwepo na mafanikio kwa vile mafanikio hayo hayakuwa kamilifu; bila kugundua kuwa ingawa sera za zama za uchumi wa pembejeo - mazao zinaweza kuwa hazijabadilika bado, "sauti" ama haja ya kuwa na mkabala mbadala tayari imeshajitokeza wazi. Hatari mbadala ni kufikiria kwamba kwa vile kuna utambuzi linganifu wa matatizo, basi kutakuwa na upatanifu vilevile wa kutatua matatizo haya. Hivyo inaonekana fursa na namna ya kusonga mbele inategemea kuzingatia mambo mawili: kwa upande mmoja kwa vile "sauti" imejitokeza na watu wako tayari kuisikiliza na kutoa ushirikiano, jitihada zaidi zinahitajika kuwekwa kwenye kipengee cha jinsi gani; kwa upande mwingine majaribio yanayohusu "jinsi gani" hayawezi kuchukulia kuwa watu waliokubaliana juu ya nini kibadilike, wana mtazamo mmoja ule ule wa namna ya kuleta mabadiliko hayo. Hivyo majaribio haya ya awali, yanayohusu mifumo ya maarifa ya asili na taasisi yatahitajika kubainisha wazi mifumo yake ya kidhana na athari zake za nguvu/udhibiti ili kwamba tofauti katika mitazamo na mikabala iweze kubainishwa na kushughulikiwa kwa makubaliano, badala ya kuendelezwa katika malumbano yasiyo kikomo. Kudhani
Huleta Tofauti Tofauti kuu katika kuleta mabadiliko hutegemea kama mtu anatarajia maendeleo ya kiuchumi na kijamii yaanzie ndani ya nchi ama yategemee msukumo toka nje. Jumuiya ya maendeleo ya kimataifa na serikali za Kiafrika ambazo zina upendeleo wa muda mrefu wa mfumo wa uchumi wa pembejeo - mazao kwa kawaida zimekuwa zikikumbatia msukumo wa maendeleo unaotoka nje. Kadiri dhana ya uendelevu ilivyoanza kutilia mkazo umuhimu wa umiliki wa washiriki na uwajibikaji unaotokana na umiliki huo, haja ya kuwashirikisha wananchi katika miradi ya maendeleo imeongezeka sana. Hapa, hata hivyo, mashirika ya wahisani aghalabu yamekuwa yakidhani kwamba harakati za ushirikishwaji zingetumika kuwaelewesha wananchi mifumo mikuu ya sasa ya kiuchumi na kiutamaduni ya nchi za magharibi - lakini kwa uangalifu zaidi na kulingana na muda wao wenyewe. Kimsingi hali hii hufanya mambo yanayodhaniwa kuhusu msukumo huu wa maendeleo toka nje yasiguswe na yasitafakariwe. Uwezekano kwamba taasisi za asili za Kiafrika - aghalabu hubainishwa kama za "kimila" ama "zisizo rasmi" - zinaweza kuwa msingi wa maendeleo yanayoanzia ndani ya nchi haujachunguzwa sana. Hata hivyo, mkazo wa sasa wa maendeleo unaolenga kuongeza uwezo wa wananchi na taasisi umeanza kutathimini upya ufanisi wa taasisi hizi. Kwa mfano, Mamadou Dia, katika makala yake "kwanini utamaduni ni muhimu" ya 1991 alipendekeza kwamba utambuzi na utumiaji wa taasisi za asili za Afrika ni muhimu katika kuleta usitawi wa bara hili. Kufuatia pendekezo hilo utafiti wa kikanda ujulikanao kama "Menejiment ya Afrika kwa ajili ya miaka ya 1990" uliandaliwa ili kuchunguza ufanisi wa kutumia taasisi za asili, hasa menejimenti na upangiliaji wa shughuli. Matokeo ya utafiti yameonyesha umuhimu wa utamaduni na taasisi za asili katika uongozi bora, hasa unaoshirikisha wananchi katika uzalishaji mali. Wakati huo huo, matokeo yameanza kuonyesha viwango vikubwa vya utengano katika taasisi zilizo rasmi na jumuiya za kiraia za Kiafrika. Hatari kubwa hapa ni ile ya kupanua kiwango kilichopo cha utengano. Uwezekano huo ni mkubwa iwapo matumizi ya mifumo ya maliasili za Kiafrika hayatakwepa athari za kigeni katika ngazi zote. Kwa upande mwingine, ingawa zipo fursa nyingi za kuziba utengano na kupanua mifumo ya maarifa ya asili, ili jambo hili lifanikiwe viunzi vya kidhana lazima vibadilike, na kazi halisi, kwa kiwango kikubwa, itakuwa tata na isiyopimika. Kubainisha
Mikakati ya Ushirikishwaji Mikabala inayotumika kushirikisha wananchi ni mingi na ina malengo, mikakati ya utekelezaji na matokeo tofauti tofauti. Tathmini ya viwango vya udhibiti na uendelevu hutoa viwango vya ushirikishaji vilivyo dhahiri zaidi. Hali hii, kwa upande wake, inatoa kipimo kinachofanya mashirika wezeshaji kuwa makweli kuhusu juhudi za ushirikishaji na matokeo yake. Uwezo huu ni muhimu hasa pale vikundi vinapoamua kuacha mifumo ya maendeleo ya nje na kuanza kutumia msukumo na taasisi za ndani ya nchi. Ili kuweka viwango vya msingi mikakati ya ushirikishaji imegawanyika katika kategoria nne. Mikakati hii imeanishwa zaidi kufuatana na kiwango cha udhibiti cha watendaji/washirika. Uimarishaji huu, ambao msingi wake ni kipimo cha nguvu/uhamishaji wa udhibiti, unaelezea jinsi mikakati ya ushirikishwaji mbalimbali inavyofanya kazi na nini inaweza kutarajia kutimiza kwa mtazamo wa " mtendaji/mshiriki" na "nguvu za nje". Mikakati ya msingi na msisitizo wa udhibiti ni kama ifuatavyo: Mkakati wa
Uhamasishaji Mradi wa maendeleo huchaguliwa na kuandaliwa na watu wa nje, kwa kawaida na wataalam wa taasisi za wahisani au serikali zilizobuni mradi, kabla ushirikishaji wa watu haujaanza. Kisha uongozi wa programu "huwahamasisha na kuwakusanya" "wafaidika walengwa" ili kuidhinisha, kushiriki na kupitisha maamuzi yaliyokwisha chukuliwa. Mkakati huu unaliachia shirika la nje udhibiti kamili. Mkakati wa
Maendeleo ya Jumuiya/Taasisi Tafiti za kijamii au mikutano hufanywa ili kupata uelewa mzuri zaidi wa mtazamo wa jumuiya/taasis kuhusu tatizo maalum lililoainishwa kuwa linakwamisha maendeleo. Vikundi vya wenyeji vinaweza kuhusishwa, kwa kutumia mbinu za ushirikishaji, katika kupanga na kutekeleza utatuzi wa tatizo. Mtendaji/washiriki huchangia kwa viwango maalum udhibiti na wakala wa nje, lakini uamuzi juu ya kiwango mahususi cha udhibiti kuamuliwa aghalabu toka nje. Mkakati wa
Kujikusanya Pamoja Vikundi vya watu waliotengwa kwa namna fulani hujikusanya pamoja, au hukusanywa ili viwe na nguvu zaidi na uwezo zaidi wa kuwaathiri wale wanaofanya maamuzi juu ya vikundi hivyo. Vyama vya ushirika, vyama vya vijijini na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) ya kwenye jumuiya, ni mifano ya mkakati huu. Mtendaji/washiriki huchangia kwa viwango maalum udhibiti na wakala wa nje au na viongozi waliochaguliwa. Mkakati wa
Uwezeshaji Vikundi vya kijumuiya, mara nyingi kwa msaada kutoka nje, huanzisha mpango wa mafunzo/uwezeshaji unaoviwezesha kuandaa malengo yao; kutathimini matokeo ya fursa mbadala zilizopo; kuamua na kuchukua hatua za kutekeleza malengo yao. Mkakati wa uwezeshaji huweka udhibiti mikononi mwa mtendaji/washiriki, ambao ndiyo wenye haki na wajibu. Kwa matokeo endelevu, swali muhimu ni: je, udhibiti unakuwa kwa nani hasa? Mkakati wa "uhamasishaji" huweka udhibiti wote mikononi mwa mameneja wa mradi na hivyo ni rahisi kuanzisha na kuusimamia. Lakini, kwa vile udhibiti wa wenyeji ni mdogo mno, mkabala huu aghalabu huhatarisha msingi wa uendelevu. "Maendeleo ya jumuiya" na "mikakati ya kujikusanya pamoja" kuchangia kiwango fulani cha udhibiti na washiriki na hivyo ina uwezo wa kuwa na uendelevu wa kutosha, lakini kwa masharti yafuatayo: (a) Kwamba usimamizi wa mradi uzingatie mitindo ya asili; na (b) zao la mradi likidhi mahitaji muhimu ya jumuiya, kama vile uimarishaji wa huduma ya upatikanaji wa maji. Mikakati ya "uwezeshaji" huwawezesha washiriki kubuni miradi yao na kuitekeleza na hivyo kuweka udhibiti na wajibu mkubwa mikononi mwa washiriki, pakiwepo na kiwango kikubwa cha uendelevu. Lakini udhibiti mkubwa mno unaweza pia kuongeza utengano. Kila moja ya mikakati hii ya ushirikishaji, licha ya kuwa na kipengee cha udhibiti, huwa pia na "kipengee cha matendo". Katika kuchagua mkakati ni muhimu kuweka wazi kipengee hiki cha matendo. Na jambo muhimu zaidi kwa mafaniko ya mradi ni kuelewa jinsi kipengee cha matendo kinavyohifadhika ama kukengeuliwa wakati wa utekelezaji. Mikakati ya uhamasishaji hutumia washiriki kupata ushauri; mikakati ya maendeleo ya jumuiya na ya kujikusanya pamoja hutumia washiriki kufanya mapatano; na mikakati ya uwezeshaji huwatumia kuanzisha kujitawala. Kuelewa kipengee cha matendo cha mikakati mbalimbali ya ushirikishwaji na pia tofauti muhimu miongoni mwake, huweza kutusaidia kuamua wapi uwekwe udhibiti kwa ajili ya uwezekano mkubwa wa uendelevu. Hatari hapa ni kwamba ili kufanya kazi kwa ufanisi kwa kutumia mifumo ya maarifa ya asili, mikakati yote miwili ya mapatano na uwezeshaji lazima itumike na iwe endelevu kwa muda mrefu, kwa ngazi za chini na pia zile za sera. Kuhifadhi mikakati hii bila kurejea nyuma kwenye ngazi za mapatano ni jambo gumu sana. Kwa upande mwingine, fursa iliyopo ni kwamba ulazima wa lengo hili utasababisha kuvumbuliwa maarifa mengi ya "jinsi gani" ambayo yatafanya juhudi za baadaye katika eneo hili kuwa rahisi zaidi kutekelezeka. Hitimisho Kwa kifupi, mikabala ya ushirikishaji inayoweza kufanya kazi vizuri na mifumo ya maarifa ya asili badala ya kupingana nayo haichanganuliwi kirahisi au kutoa utatuzi rahisi wa matatizo. Hata hivyo, ushirikishaji huu hukabili vema utata na utegemeano wa masuala menyewe. Aidha huelekeza kwa ufanisi mbinu zinazohitaji kutatua matatizo kwa ajili ya kupata masuluhisho endelevu. Lakini jambo la muhimu zaidi ni kwamba hii ni hatua ya kwanza ya kurejesha maendeleo ya Afrika kwenye msukumo wa ndani badala ya ule unaotoka nje ya bara la Afrika. Makala hii imerekebishwa na Paula Donnelly - Roark kutokana na makala "Perspectives on Indigineous Knowledge Systems in Southern Africa" ya Jeri Larson, 1998, katika Discussion Paper No.3, Invironment Group, Africa Region, World Bank. Kwa maelezo zaidi juu ya makala wasiliana na: Ms Paula Donnelly - Roark, Rm. J2 - 115, WB, 1818 H Street NW, Washington D>C 20433. Tel (202) 4737574 E-mail:
Pdonnellyroark@worldbank.org |